Jan 14, 2022 03:12 UTC
  • Yemen yakosoa utendaji wa Baraza la Usalama katika kurefusha vita vya nchi hiyo

Muhammad Ali al-Huthi, mwanachama wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amekosoa utendaji wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya kivamizi dhidi ya nchi hiyo na kusema licha ya kwamba Saudi Arabia imetekeleza na inaendelea kutekeleza jinai za kivita nchini humo, lakini baraza hilo limeshindwa kusimamisha vita hivyo.

Vita vya Yemen vilianza mwaka 2015 ambapo kufikia nusu ya mwaka uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa limepitisha maazimio 17 kuhusiana na mgogoro huo. Licha ya mazimio hayo yote lakini Baraza la Usalama limeshindwa kusimamisha vita vya kivamizi vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen, jambo ambalo limeamsha hasira na malalamiko ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen. Hivi karibuni pia Hisham Sharaf, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali hiyo, alimwandikia barua Abdu Abadi, mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Usalama.

Katika barua hiyo Hisham Sharaf amesema ni wazi kuwa Saudia alianzisha vita vya kivamizi dhidi ya Yemen na kuwa ni jambo la kusikitisha na kushangaza kuona kwamba Baraza la Usalama na jamii ya kimataifa imeketi kimya na kutochukua hatua yoyote ya kulaani jinai za nchi vamizi. Amesema inaumiza hata zaidi kuona kuwa jamii hiyo hiyo hukerwa inapoona  kwa serikali ya Sanaa inachukua hatua za kisheria kimataifa na kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa katika kujitetea na kutetea watu wake.

Muhammad Ali al-Huthi

Nukta muhimu ni kwamba, maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa si tu hayajakuwa na taathira yoyote ya maana katika kupunguza mgogoro wa Yemen bali hata yamechangia katika kurefusha mgogoro huo. Hii ni kwa sababu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen yamekuwa yakiunga mkono wazi wazi matashi na maslahi ya kisiasa na kupuuza haki za msingi za watu wa Yemen, ambapo yamekuwa yakitoa upendeleo maalum kwa serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi na kulaani harakati ya Ansarullah pamoja na washirika wake na wakati huo huo kutoashiria kwa namna yoyote ile jinai zinazofanywa na muungano wa vamizi wa Saudia dhidi ya Wayemen.

Licha ya kuwa mitazamo ya kisiasa katika maazimio ya Baraza la Usalama ni jambo la kawaida na linalokaririwa mara kwa mara lakini ambalo lilidhihirisha zaidi mitazamo na maslahi hayo ya kisiasa ni lile lililopitishwa tarehe 14 Aprili mwaka 2015. Azimio hilo nambari 2216 lilipitishwa kwa kura 21 za ndio na moja ya hapana ambayo ilikuwa ya Russia.

Azimio hilo liliilaani Ansarullah katika hali ambayo ni Saudia ndiyo ilianzisha vita vya kivamizi dhidi ya Yemen. Nukta muhimu katika azimio hilo ni kwamba badala ya Baraza la Usalama kulaani uvamizi wa Saudia dhidi ya nchi jirani ni Ansarullah ndiyo ililengwa kidhulma na azimio hilo lililochochewa na nchi za Magharibi zikioongozwa na Marekani. Jambo jingine ni kwamba azimio hilo hata halikutaka mashambulio ya mabomu dhidi ya Yemen yasimamishwe. Azimio hilo ndilo limekuwa msingi wa maamuzi yote yanayochukuliwa na Baraza la Usalama kuhusiana na Yemen katika kipindi cha miaka 7 iliyopita.

Maudhui nyingine ni kwamba Baraza la Usalama halikuiwekea Saudia ambayo ni mvamizi wa Yemen na mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika nchi hiyo masikini, aina yoyote ya vikwazo bali nchi za Magharibi zinazoiunga mkono kwa hali na mali, zinaendelea kuiuzia kila aina ya silaha za kisasa kwa ajili ya kuendeleza vita vyake vya kichokozi dhidi ya watu wa Yemen.

Shule ya watoto wa Yemen iliyoharibiwa katika uvamizi wa Saudia

Katika uwanja huo tunaweza kuashiria mkataba wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 110 uliotiwa saini mwezi Mei 2017 kati ya Marekani na Saudia.

Nukta ya mwisho ni kwamba licha ya kuwa Baraza la Usalama ni baraza lililo na wanachama huru lakini ni wazi kuwa misimamo inayokinzani ya wanachama hao hupelekea baraza hilo lisiweze kutekeleza vizuri majukumu yake, kutokana na kura ya veto waliyonayo wanachama wa kudumu wa baraza hilo.