Jan 15, 2022 07:25 UTC
  • Sababu za idadi kubwa ya vifo vya wanajeshi wa Israel

Gazeti la Kiebrania la Israel Hume limeripoti kwamba wanajeshi 31 wa Israeli waliuawa katika mwaka uliomaliza majuzi wa 2021 na kwamba 11 kati yao walijiua wenyewe.

Kumetajwa sababu kadhaa za vifo vya wanajeshi wa Israel. Sababu kuu ya kuuawa wanajeshi wa Israel inahusiana na siasa za kijeshi za utawala huo ghasibu. Utawala wa Israel kimsingi ni utawala unaopenda vita. Kwa msingi huo, kama ambavyo siasa za kivita za utawala huo ghasibu husababisha kuuawa shahidi wanajeshi na raia wa nchi zinazolengwa hususan Palestina, vilevile zinapelekea kuuawa wajeshi wa Israel. Katika mkondo huo, katika vita vya siku 12 vya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mwezi Mei 2021, Waisraeli 12 waliuawa na wengine 330 walijeruhiwa. 

Askari wa Israel 

Taathira za vita kawaida haziishii katika mapigano ya kijeshi, bali zimekuwa madhara na hasara kubwa za kijamii na kinafsi kwa wanajeshi wa utawala haramu wa Israel. Idadi kubwa ya askari wa utawala huo wamepatwa na ugonjwa wa sonona na mfadhaiko kutokana na vita mtawalia na kukosa usalama wa ajira na kazi, masuala ambayo yanawasukuma kujiua. Gazeti la Kiebrania la Israel Hume limeripoti kwamba, wanajeshi 11 wa Israeli walijiua wenyewe mwaka uliopita wa 2021. 

Kuongezeka kwa mivutano kati ya wanajeshi kunatajwa kuwa ndio sababu kuu ya kujiua huko, na suala hili linahusiana na mashinikizo ya kisaikolojia, kijamii, kiusalama, vita na makabiliano ya mara kwa mara. Hakuna takwimu kamili juu ya idadi ya wanajeshi wa Israeli ambao wamekuwa waraibu wa dawa za kulevya, lakini uraibu pia ni sababu kuu ya matatizo ya kijamii na vitendo vya kujiua vya wanajeshi wa Israel. Kuanzia mwaka 2010 hadi 2020, takriban watu 5,380 walifanya majaribio ya kujiua huko Israel, ambayo ni takriban watu 500 kila mwaka na 100 kati yao walikuwa wanajeshi. Kituo cha habari cha Palestine Today kimeripoti kuwa: "Wanajeshi wengi wa Israel ambao wamejiua wameteseka kwa muda mrefu kutokana na wasiwasi wa siku zijazo, kukata tamaa na kuchanganyikiwa. Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2020 maombi 1,710 yaliwasilishwa na wajeshi wakiomba huduma za afya ya akili, na majina ya wanajeshi 26 miongoni mwao yalisajiliwa katika orodha ya wagonjwa wanaosumbulia na hatari kubwa na zilifanyika juhudi za kuwaokoa ili wasijiue."

Mapigano kati ya wanajeshi wa Israel, wao kwa wao, ni sababu nyingine ya vifo vya wanajeshi wa utawala huo haramu. Matatizo ya kisaikolojia mara nyingi husababisha ugomvi na migogoro kati ya wanajeshi wa Israel, na kuzusha mapigano na ghasia kutokana na wanajeshi hao kutokua na mlingano wa kiakili. Katika mkondo huo, vyombo vya habari vya Israel vimechapisha ripoti nyingi za mapigano kati ya wanajeshi wa utawala huo ghasibu.

Matukio ya ajali ni miongoni mwa sababu muhimu za vifo vya wanajeshi wa Israel. Vifo vinavyotokana na majanga ya asili, ikiwa ni pamoja na ajali za barabari, vinaripotiwa kuwa vingi kati ya wanajeshi wa Israel.

Maradhi pia yanatajwa kuwa miongoni mwa sababu kubwa za vifo vya wanajeshi Wazayuni. Katika miaka miwili iliyopita, virusi vya corona haswa vimekuwa sababu kuu ya vifo vya wanajeshi wa utawala huo haramu. Kuhusiana na hilo, Kamanda wa Wafanyakazi wa Jeshi la Israel, alitangaza kwamba idadi kubwa zaidi ya vifo vya wanajeshi wengi wa jeshi la Israel katika mwaka wa 2021 vilitokana na maradhi na kwamba baadhi yao wameuawa na COVID-19.

Nukta ya mwisho ya kuashiria hapa ni kwamba, maafisa wa Israel hawatoi takwimu halisi juu ya idadi ya wanajeshi waliouawa au kufa kifo cha kawaida katika kipindi cha mwaka mzima.   

Tags