Jan 15, 2022 08:08 UTC
  • Jihadul-Islami: Muqawama utaendelea kuunga mkono Intifadha ya wakazi wa Ufukwe wa Magharibi

Msemaji wa Harakati ya Jihadul-islami ya Palestina amesema, muqawama unaunga mkono intifadha na mwamko wa wakazi wa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya wazayuni.

Tariq Izzuddin ametoa msimamo huo kutokana na kushtadi hatua za kiuadui za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wakazi Wapalestina wa eneo la An-Naqb katika Ufukwe wa Magharibi.

Izzuddin ameongezea kwa kusema, ukweli ni kwamba utawala wa Kizayuni hautaacha kufanya jinadi dhidi ya Wapalestina, kwa hiyo inapasa litumike chaguo la muqawama ili kukabiliana nao, kwani utawala huo hautaweza kudumu kukabiliana na muqawama.

Msemaji wa Jihadul-Islami amekumbusha kuwa jamii ya kimataifa imenyamazia kimya jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa An-Naqb na kwamba wakati wazayuni wanawahamisha kwa nguvu wakazi wa An-Naqb kwenye makazi yao, wanaofanya mapatano na Israel katika ulimwengu wa Waarabu nao pia ni washirika wa uhalifu huo.

Uvamizi wa askari wa Kizayuni Ufukwe wa Magharibi

Kwa siku kadhaa sasa askari wa utawala dhalimu wa Kizayuni wamevamia vijiji kadhaa vya eneo la An-Naqb kwa lengo la kuharibu ardhi za kilimo za wakazi wenyeji wa maeneo hayo na kuzipora ardhi hizo kwa ajili ya kuanzisha ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Wapalestina zaidi ya 100 wakiwemo wanawake na wasichana wadogo wamekamatwa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika uvamizi huo.../

Tags