Jan 15, 2022 12:13 UTC
  • Kambi ya jeshi la US nchini Iraq yashambuliwa kwa droni

Uwanja wa ndege za kijeshi wa Marekani wa Balad ulioko kaskazini mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad umeshambuliwa kwa ndege zisizo na rubani.

Ukurasa wa habari wa Sabereen kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram unaohusishwa na Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq maarufu kama Hashd al Sha'abi umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, droni kadhaa zimetumika katika mashambulio hayo dhidi ya kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani, yapata kilomita 64 kaskazini wa Baghdad.

Sauti za ving'ora zimesikika huku wingu zito la moshi likifuka kutoka kwenye kituo hicho chenye askari, ndege za kivita na zana za kijeshi za Marekani, kilichoshambuliwa mapema leo Jumamosi.

Mrengo wa muqawama nchini Iraq umeapa kuendeleza hujuma dhidi ya kambi na vituo vya askari vamizi wa Marekani ndani ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu, hadi watakaposalimu amri na kuondoka.

Vikosi vamizi vya Marekani nchini Iraq

Mapema mwezi huu, duru za habari za Iraq ziliripoti habari ya kushambuliwa kwa roketi kambi ya Ainul-Asad ambayo ni makao ya wanajeshi wa Marekani.

Kundi moja la Kiiraqi liitwalo Qaasimul-Jabbarin lilitangaza rasmi katika taarifa kwamba ndilo lililoshambulia kituo hicho cha anga kilichoko mkoani Al Anbar, magharibi mwa nchi hiyo.

Tags