Jan 16, 2022 12:32 UTC
  • Baa la njaa nchini Afghanistan

Zaidi ya watu milioni 22 nchini Afghanistan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Kukosekana misaada ya kimataifa sambamba na ukame ulioambatana na kupanda pakubwa bei za bidhaa hasa vyakula, ni mambo ambayo yameifanya Afghanistan ijongewe na baa kubwa la njaa na kuitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro na matatizo makubwa ya ukosefu wa chakula.

Kwa kuzingatia kuwadia msimu wa baridi na kuweko haja kubwa ya nishati ya mafuta, hapana shaka kuwa, matatizo ya Afghanistan yamekuwa maradufu na kuchukua wigo mpana zaidi. Moja ya sababu kuu zinazoifanya nchi hiyo iendelee kukumbwa na matatizo ya uhaba wa chakula ni upuuzaji wa Marekani na mataifa ya Ulaya wa kuleta na kuimarisha miundomsingi ya kiuchumi na kilimo ya Afghanistan katika kipindi cha miongo miwili ya kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo na majeshi ya Marekani.

Watoto nchhini Afghhanistan ni wahanga wakuu wa njaa na ukosefu wa usalama

 

Hii ina maana kwamba, katika kipindi cha miongo miwili iliyopita ya kuweko kijeshi Marekani na washirika wake huko Afghanistan, siyo tu kwamba, wahusika hawakuchukua hatua za kuboresha hali ya kiuchumi na kimaisha ya wananchi wa nchi hiyo, bali walitekeleza mipango iliyoratibiwa na kuifanya nchi hiyo iwe tegemezi wa misaada yao. Filihali, Marekani imeondoka nchini Afghanistan na ikiwa na lengo la kuwatia adabu wananchi wa nchi hiyo imekataa kuachilia fedha za Afghanistan zilizoko nchini Marekani licha ya kutakiwa mara kadhaa iachilie fedha hizo ili ziwasaidie wananchi hao hasa katika kipindi hiki kigumu cha kiuchumi.

Ramiz Alac mtaalamu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya chakula anaamini kuwa, takribani theluthi moja ya wakazi milioni 38 wa Afghanistan wanakabiliwa na hali ya dharura na mgogoro wa chakula unaondelea na kwamba, kunahitajika mabilioni ya dola kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo.

Mbali na jinai za Marekanui na washirika wake huko Afghanistan, serikali zilizotangulia iwe ni katika kipindi cha uongozi wa Hamid Karzai au Muhammad Ashra Ghani, siyo tu hazikuchukua hatua za kuboresha miundombinu ya nchi hiyo na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi, bali Afghanistan ilisakamwa na mizozo ya kikaumu na ufisadi wa kiidara na kifedha masuala ambayo yanaweza kuwa na taathira hasi kwa nchi hiyo hata katika miaka ijayo.

Wakimbizi wa Afghanistan

 

David Bizly, mtaalamu wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP) anaamini kuwa, siku za kutokea maafa ya kibinadamu nchini Afghanistan zinmeanza kuhesabika na kama hatutachukua hatua za maana za kukabiliana na jambo hilo, kutatokea maafa kamili ya kibinadamuu nchini humo.

Vyovyote itakavyokuwa, kuibuka matatizo ya chakula na baa la njaa nchini Afghhanistan, kunazidi kuweka wazi khiyana na jinai za serikali zilizotangulia nchini Afghanistan pamoja na wavamizi dhidi ya wananchi wa nchi hiyo. Katika mazingira haya inaonekana kuwa, tawala za Maghharibi na asasi za kimataifa zenye mfungamano na tawala hizo zinapaswa kuchukua hatua za kuwasaidia wananchi wa Afghanistan waweze kujikwamua na tatizo la chakula.

Kwa muktadha huo, katika mazingira haya mataifa ya Kiislamu hususan Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ina jukumu zito la kusaidia kupatiwa ufumbuzi tatizo la uhaba wa chakula nchini Afghanistan na kuhitimisha hali mbaya ya kimaisha na mgogoro wa chakula unaowakabili wananchi wa nchi hiyo.

Tags