Jan 17, 2022 09:17 UTC
  • Iran yasisitiza ulazima wa kuondolewa mzingiro wa kidhalimu wa Yemen

Ali Asghar Khaji, Mshauri Mwandamizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Hans Grundberg, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, wamefanya mazungumzo ya simu wakijadili matukio ya hivi karibuni nchini Yemen.

Akiashiria hali ya kusikitisha ya wananchi wa Yemen na hali ngumu sana inayotokana na vita na mzingiro wa kidhalimu wa kiuchumi, mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kwa ujumla ifanyike juhudi kubwa za kusimamisha vita hivyo na kuondoa mzingiro wa Yemen. Ali Asghar Khaji amesema kuwa kuondolewa mzingiro wa kidhalimu dhidi ya watu wa Yemen ndio utangulizi wa kupatikkana utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa nchi hiyo. 

Mohammad Amin Hatit, mtaalamu wa masuala ya kimkakati ya eneo la Asia Magharibi amezungumzia kushindwa vibaya kwa Saudi Arabia katika vita vya Yemen na kusema: "Mwaka wa 2015, mtawala wa Saudi Arabia alianzisha vita hivyo vyenye uharibifu mkubwa chini ya anwani ya 'Tofani Madhubuti' dhidi ya Wayemeni. Saudi Arabia ilifikiri kwamba, kutimiza malengo yake katika vita hivyo ni kazi rahisi na kwamba operesheni ya utawala huo ya kutaka kutwaa utajiri wa mafuta na gesi wa Yemen na kudhibiti eneo la Bab al-Mandeb na Bahari ya Shamu itachukua wiki chache tu. Sera hii ya kupenda makuu ya Saudi Arabia iliimarishwa kwa himaya ya Marekani na Uingereza kiasi Wasaudia walikuwa kwenye ndoto kwamba, wana nguvu kubwa kwa kadiri kwamba hakuna mtu anayeweza kusimama mbele yao."

Waislamu waliouawa kwa mashambulizi ya Saudia wakiwa msikitini..

Saudi Arabia na washirika wake wameendeleza vita dhidi ya Yemen kwa kutumia dhana na mahesabu haya potofu na yasiyo sahihi. Hata hivyo harakati ya muqawama na mapambano ya watu wa Yemen imeonesha kuwa, Saudi Arabia haitafikia malengo yake ya kijeshi, na kwamba mzingiro na mauaji dhidi ya watu wa Yemen havitavunja irada na azma ya taifa hilo. Vita vya Yemen kwa hakika ni vita vilivyoshindwa na vya gharama kubwa kwa Saudi Arabia, na kadiri wakati unavyosonga mbele katika vita ndivyo muungano wa Saudia na Marekani unavyopata hasara na vipigo zaidi. Kujiondoa kwenye kinamasi hicho kutategemea uamuzi wa kimantiki na jibu kwamba je, Saudi Arabia iko tayari kuchukua uamuzi wa kimantiki au la? Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, maamuzi matatu ya kimkakati yanahitajika ili kuondokana na mkwamo huu: 

Kwanza ni kusimamisha na kukomesha kabisa vita na mzingiro wa Yemen. 

Pili ni kushirikiana ipasavyo na Umoja wa Mataifa katika kadhia ya nchi hiyo. 

Stratijia ya tatu ni kurejea kwenye msingi wa kujenga hali ya kuaminiana na kuheshimu kanuni ya kuwapa Wayemeni haki ya kujiamulia hatima ya masuala ya kisiasa ya nchi yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian alisema katika mahojiano yake ya hivi karibuni na televisheni ya Al-Jazeera kwamba, hali ya Yemen inatia wasiwasi na kuongeza kuwa: "Imepita karibu miaka sita sasa tangu kuanza kwa vita na uvamizi dhidi ya Yemen. Suala hili mbali na kwamba ni dhulma dhidi ya watu wa Yemen lakini pia Saudi Arabia kama nchi ya Waislamu, imeamua kutumia rasilimali zake kwa ajili ya vita badala ya kuzitumia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi za Kiislamu. Nchi zinazofaidika na hali hii ni zile zinazoiuzia Saudia silaha na zana za kivita ambazo daima zinataka kuzusha moto za fitina na mapigano katika eneo la Magharibi mwa Asia."

Hossein Amir-Abdollahian

Kilichotokea katika kipindi cha karibu miaka 7 ya mashambulizi ya Saudia huko Yemen ni jinai za kivita na mauaji ya halaiki ya watu wasio na hatia wa Yemen. Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zaidi ya nusu ya Wayemeni wanasumbuliwa na njaa, na kwa sasa nchi hiyo inakumbwa na maafa makubwa zaidi duniani.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza udharura wa kutafuta suluhisho la kisiasa la vita hivyo vya kidhalimu. Iran, kama mchezaji muhimu na mwenye taathira katika siasa za eneo hili, itatumia uwezo wake wote wa kidiplomasia na uhusiano wa kikanda katika mwelekeo huu.