Jan 17, 2022 17:05 UTC
  • Watu 9 wauawa na kujeruhiwa nchini Imarati baada ya mashambulizi ya Wayemen

Ndege 20 zisizo na rubani pamoja na makombora 10 ya balestiki ya Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen yameshambulia maeneo muhimu na nyeti ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti habari hiyo na kusema kuwa, shambulio hilo limetokea leo Jumatatu ambapo kwa mujibu wa ripoti hiyo, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na Ansarullah limeshambulia ndani kabisa ya ardhi ya UAE kwa kutumia ndege 20 zisizo na rubani na makombora 10 ya balestiki. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kwa uchache watu watatu wameuawa na wengine 6 kujeruhiwa katika shambulio hilo la kulipiza kisasi.

Televisheni hiyo imesema pia kwamba shambuio hilo limefanyika ndani ya mji mkuu wa Imarati yaani Abu Dhabi na moshi pamoja na miale ya moto imeonekana ikielekea juu baada ya mashambulio hayo.

Picha ya Middle East Eye inayoonesha moshi mzito baada ya mashambulio ya Jeshi la Yemen mjini Abu Dhabi, UAE.

 

Kabla ya hapo, Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree aliuonya Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa uache kuuwa wananchi wa Yemen vinginevyo San'a italipiza kisasi kwa nguvu zake zote ndani ya ardhi ya Imarati.

Kabla ya kuenea habari hii pia, msemaji huyo wa Jeshi la Yemen alikuwa ameahidi kutangaza habari muhimu kuhusu operesheni maalumu iliyofanywa na Wayemen ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mchana wa leo Jumatatu shirika la habari la Imarati WAM limetangaza habari ya kutokea miripuko miwili karibu na maghala ya mafuta na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abu Dhabi, mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu. 

Tags