Jan 18, 2022 01:46 UTC
  • Malalamiko ya Palestina kwa kimya cha ulimwengu kuhusu sera za apartheid za Israel

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetoa taarifa ikilalamikia kimya cha taasisi za kimataifa duniani mkabala wa uvamizi na chokochoko za utawala ghasibu wa Israel hususan ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala huo na kusema kuwa, Tel Aviv inataka kuimarisha ubaguzi wa Apartheid dhidi ya Wapalestina.

Kifungu cha pili cha Mkataba wa Kimataifa unaopiga marufuku na kutoa adhabu kwa jinai za ubaguzi wa Apartheid kinaeleza kuwa: "Apartheid ambayo ni sera na vitendo sawa na vile vya kutenganisha watu kwa msingi wa mbari zao na ubaguzi wa kimbari na kikaumu vilivyoshuhudiwa nchini Afrika Kusini, ni vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyotekelezwa na kundi la watu wa mbari moja dhidi ya mbari nyingine na kulidhulumu kundi hilo kupitia mfumo maalumu." 

Aidha kipengee cha kwanza na cha pili cha kifungu cha kwanza cha mkataba huo kinaeleza kuwa, nchi zinazounga mkono mkataba huo zinatangaza waziwazi kwamba, apartheid ni jinai dhidi ya binadamu na tishio kubwa kwa amani na usalama wa dunia, na kwamba nchi hizo zinazitambua taasisi, jumuiya na watu wanaotenda jinai ya apartheid kuwa ni wahalifu. 

Vitendo na hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina ni kielelezo cha wazi cha ubaguzi wa apartheid. Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina na kwa kupuuza azimio nambari  2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni kati ya mifano ya wazi ya jinai za apartheid zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema katika ripoti yake kwamba: Utawala wa Kizayuni wa Israel unapoteza wakati ili kufanikisha miradi yake ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi na ukoloni wake katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Si hayo tu, bali utawala huo umekusudia kufanya mabadiliko makubwa katika hali ya kihistoria na kisheria ya eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ili hatimaye ufunge kabisa milango na uwezekano wa kuundwa nchi huru ya Palestina, mji wake mkuu ukiwa Quds.   

Utawala haramu wa Israel unatekeleza miradi ya upanuzi wa vitongoji vya walowezi lengo kuu likiwa ni kuyayahudisha maeneo unayoyakalia kwa mabavu ya Palestina. Ujenzi wa vitongoji hivyo na kuyayahudisha maeneo ya Palestina kunabadili pia utamaduni wa maeneo hayo. Baada ya kutekeleza mipango hiyo ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, Baraza la Mawaziri la utawala wa Israel tayari limebuni sheria ambazo zinawatesa na kuwabughudhi raia wa Palestina waliosalia katika maeneo hayo na kuyafanya mazingira hayo kuwa magumu sana kwao kimaisha. Israel inapora na kutwaa kwa mabavu nyumba na ardhi zinazomilikiwa na Wapalestina na kuwatenganisha raia hao kwa misingi ya mbari, kaumu na dini yao na wakazi wengine wa vitongoji vinavyokaliwa kwa mabavu; hatua ambayo ni mfano wa wazi wa jinai ya apartheid. 

Hadi kufikia sasa, taasisi mbalimbali za kimataifa zimezitaja jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa jinai hiyo ya kujenga vitongoji vya walowezi katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina kuwa ni kielelezo cha apartheid. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti  kamili iliyojumuisha uchambuzi mkubwa wa kisheria na kueleza kuwa: Maafisa wa Kizayuni wa Israel wametenda jinai dhidi ya binadamu dhidi ya Wapalestina kupitia mfumo wa apartheid na kuwanyanyasa raia wa Palestina. Human Rights Watch na mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu yameashiria vielelezo vingine vya sera za ubaguzi na apartheid za utawala wa Israel na kusema: Kuendelea kunyakua ardhi za Palestina, sheria za ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zinazowatambua  Mayahudi kuwa watu bora zaidi, kadhalika kuanzishwa mfumo wa udhibiti wa Wazayuni dhidi ya Wapalestina ni mojawapo ya vielelezo hivyo. 

Kwa kuzingatia hali hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imelaani uonevu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa ni pamoja na kuharibu nyumba za makazi ya raia, maangamizi ya kizazi, ukandamizaji na manyanyaso dhidi ya Wapalestina, na kusema vitendo hivyo vya kikoloni vinakamilisha mfumo wa ubaguzi wa apartheid huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Vilevile imeitaka jamii ya kimataifa kuwashinikiza Wazayuni ili wakomeshe vitendo na shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi ya Palestina.

Jambo la msingi ni kwamba, hii si mara ya kwanza kwa Wapalestina kuitaka jumii ya kimataifa ichukua hatua madhubuti za kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni; hata hivyo kuzembea kwa taasisi za kimataifa zenye ushawishi hususan Baraza la Usalama na uungaji mkono wa madola makubwa vimeufanya utawala huo upuuze sheria na kanuni za kimataifa na kuendeleza uhalifu na jinai zake. 

Tags