Jan 18, 2022 03:15 UTC
  • Muungano vamizi wa Saudia waushambulia mji mkuu wa Yemen, Sana'a

Duru za habari jana usiku ziliripoti kuwa ndege za kivita za muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia zimefanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu wa Yemen, Sana'a.

Televisheni ya al Masira imeripoti kuwa, ndege za kivita za muungano vamizi Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia jana usiku zimeyashambulia maeneo kadhaa  kandokando ya bustani ya Septemba 21 na hospitali ya Azal katika mji mkuu Sana'a. Ripoti nyingine zinasema kuwa watu sita wameuawa hadi sasa na wengine wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo. 

Muungano vamizi wa Saudia umefanya mashambulizi yake hayo ambapo jana Jumatatu jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi yalitekeleza mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo muhimu ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kusababisha mlipuko karibu na maghala ya kuhifadhia mafuta ya Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Abu Dhabi (ADNOC)) na mlipuko mwingine katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abu Dhabi. 

Shambulio la jeshi la Yemen huko Abu Dhabi, Imarati 

Shirika la habari la Imarati limetangaza kuwa, watu watatu wamepoteza maisha na wengine sita wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo. Polisi ya Abu Dhabi pia imetangaza kuwa raia mmoja wa Pakistan na Wahindi wawili wameuawa katika mashambulizi hayo.