Jan 18, 2022 11:09 UTC
  • Mashambulio ya Wayamen dhidi ya Imarati; malengo na umuhimu wake

Jumatatu ya jana tarehe 17 Januari, ndege 20 zisizo na rubani pamoja na makombora 10 ya balestiki ya Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen zilishambulia maeneo muhimu na nyeti ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Televisheni ya al-Mayadeen imeripoti habari hiyo na kusema kuwa, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na Ansarullah limeshambulia ndani kabisa ya ardhi ya Imarati kwa kutumia ndege 20 zisizo na rubani na makombora 10 ya balestiki. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kwa uchache watu watatu wameuawa na wengine 6 kujeruhiwa katika shambulio hilo la kulipiza kisasi.

Aidha ndani ya Yemen, ndege ya mizigo ya kijeshi mali ya jeshi la Imarati imelengwa katika Uwanja wa Ndege wa Ataq katika mkoa wa Shab'wah kusini mwa Yemen. Mashambulio hayo ya Wayamen dhidi ya Imarati yanaweza kutathminiwa katika nukta kadhaa.

Mosi; mashambulio haya yamefanyika baada ya maonyo na indhari kadhaa za Wayamen dhidi ya Imarati. Licha ya kuwa serikali ya imarati Februaria mwaka 2020 ilitangaza kuondoa askari wake huko Yemen, lakini nchi hiyo iliendeleza uingiliaji wake wa kisiasa katika masuala ya ndani ya Yemen na vilivile katika miezi ya hivi karibuni imeongeza kasi ya harakati zake za kijasusi katika nchi hiyo.

Picha ya Middle East Eye inayoonesha moshi mzito baada ya mashambulio ya Jeshi la Yemen mjini Abu Dhabi, UAE.

 

Ni kwa msingi huo ndio maana viongozi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen wakaionya Imarati kuhusiana na matokeo mabaya ya kuendeleza siasa zake hizo. Muhammad al-Bukhaiti, Mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Answarullah ya Yemen hivi karibuni aliionya Imarati na kuitaka iachane na siasa zake chafu za kuzusha machafuko na mizozo kwani kama mwenendo huo utaendelea, basi Yemen italazimika kushambulia ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Kwa muktadha huo, mashambulio ya jana yalikuwa ni kutekeleza kivitendo indhari na onyo la hapo kabla ambalo Imarati ilipatiwa na Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen. Muhammad Abdul-Salam, msemaji wa Ansarullah ya Yemen na Mkuu wa Timu ya Mazungumzo ya Sana’a naye akitoa radiamali yake kwa operesheni ya jana dhidi ya Imarati ametangaza kuwa, nchi ndogo katika eneo ambayo inajitolea roho yake kwa ajili ya kuihudumia Marekani na utawala haramu wa Israel imedai kwamba, imeondoka nchini Yemen, lakini hivi karibuni imethibiti kinyume kabisa na madai ya taifa hilo.

Pili; katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Umoja wa Falme za Kiarabu umeufungulia njia utawala haramu wa Israel huko kusini mwa Yemen ambapo hivi karibuni kumeanza kujengwa kambi ya kijeshi nchini Yemen. Duru za Yemen zimetangaza kuwa, kambi hiyo ya kijeshi mali ya Israel inatarajiwa kujengwa katika Kisiwa cha Abdelkuri kilichoko katika majimui ya visiwa vya Socotra. Imarati imeanza kujenga kambi hiyo ya kijeshi kwa uratibu na Shirika la Kijasusi la utawala huo ghasibu.

Makombora ya Wayamen 

 

Inaonekana kuwa, dhana ya Imarati ni hii kwamba, kupitia kivuli cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel itaweza kwa urahisi kusukuma mbele gurudumu la siasa zake za uingiliaji masuala ya ndani nchini Yemen. Hivi karibuni Wayamen waliikamata meli ya Imarati katika maji ya Yemen iliyokuwa imesheheni silaha. Shambulio la jana katika ardhi ya Imarati linahesabiwa kuwa jibu kali la Wayamen la kupinga ushirikiano wa Abu Dhabi na utawala haramu wa Israel kusini mwa Yemen.

Tatu; katika mashambulio ya jana miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni eneo la viwanda na Uwanja wa Ndege wa Abu Dhabi ambayo yalishambuliwa kwa ndege zisizo na rubani pamoja na makombora ya balestiki. Kimsingi ni kuwa, Wayamen wamefikia utambuzi huu kwamba, uchumi wa nchi yao ni wenye kudhurika mno mkabala wa kila aina ya ukosefu wa usalama.

Wanamapambano wa Ansarullah ya Yemen

 

Ni kwa msingi huo ndio maana wamechukua hatua ya kuyalenga maeneo ya kiuchumi ya Imarati. Kanali ya Televisheni ya Russia al-Yaum sambamba na kuashiria katika ripoti yake umuhimu wa eneo la kiviwanda la al-Misfah huko Abu Dhabi imeripoti kwamba: Eneo hilo linapatikana kusini mwa Abu Dhabi na linahesabiwa kuwa moja ya maeneo muhimu kabisa ya kiuchumi nchini Imarati. Akthari ya mashirika ya kiviwanda na utengenezaji magari yanapatikana katika eneo hilo ambapo mbali na bandari ya kale kabisa ya nchi hiyo kupatikana katika eneo hilo, kuna maduka makubwa ya uuzaji magari pamoja na vituo vya kukarabati magari na kuhifadhia magari yenye nembo za kimataifa kama Bentley, Porsche na Volkswagen.

Uwanja wa Ndege wa Abu Dhabi nao una umuhimu wa kistratejia kwa nchi ya Imarati. Kulengwa kwa mashambulio maeneo hayo na Wayamen ni indhari na onyo la kivitendo kwa Imarati. Akizungumza na Kanali ya Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, Muhammad al-Bukhaiti, Mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Answarullah ya Yemen  ametangaza kuwa, kama Imarati itaendele na mashambulio yake dhidi ya Yemen, basi ijiandae kukabiliwa na mashambulio makubwa na ya kuumiza zaidi.

Tags