Jan 18, 2022 13:28 UTC
  • Yemen: Kama Imarati itaendelea kuua watu wetu, tutasambaratisha uchumi wake

Kamanda Mkuu wa majeshi ya Yemen ameionya vikali nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kusisitiza kuwa, kama Abu Dhabi itaendelea kushiriki katika mashambulizi na jinai dhidi ya wananchi wa Yemen, basi wanamapambano wa Yemen watasambaratisha uchumi wa UAE unaotegemea uwekezaji wa kigeni.

Mahdi al-Mashat ambaye pia ni Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema hayo baada ya operesheni ya jeshi na vikosi vya kujitolewa vya wananchi wa Yemen katika maeneo muhimu na nyeti ya Umoja wa Falme za Kiarabu na kusisitiza kuwa, uchumi wenye nguzo tete wa Imarati utasambaratishwa kabisa iwapo Abu Dhabi itaendelea kuua raia wa Yemen.

Al-Mashat pia amesema, iwapo Umoja wa Falme za Kiarabu utaendelea kushirikiana na wavamizi wengine wa Yemen kuwaua kidhulma wananchi wa nchi hiyo na kuendelea na njama za kulikalia kwa mabavu taifa hilo, basi wavamizi hao wasubiri majibu makali kutoka kwa wanamapambano mashujaa wa Yemen.

Moshi mzito baada ya shambulio la Wayemen mjini Abu Dhabi, Imarati

 

Mkuu huyo wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ameashiria mashambulio ya ulipizaji kisasi yaliyofanyika dhidi ya maeneo nyeti na muhimu ya mji mkuu wa Imarati, Abu Dhabi na kusema kuwa hiyo ni haki ya kisheria ya wananchi wa Yemen kujihami na kulipiza kisasi kwa kila anayewashambulia kidhulma.

Jana Jumatatu ndege 20 zisizo na rubani pamoja na makombora 10 ya balestiki ya Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen yalishambulia maeneo muhimu na nyeti ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kwa uchache watu watatu wameuawa na wengine 6 kujeruhiwa katika shambulio hilo la kulipiza kisasi.