Jan 19, 2022 03:02 UTC
  • Saudia yaua raia wa Yemen, ikiwemo familia nzima, katika hujuma dhidi ya Sana'a

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen amesema muungano wa kivita wa Saudi Arabia umetekeleza mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa Yemen, Sana'a, ambapo raia 20, ikiwemo familia moja wameuawa.

Taarifa zinasema ndege za kivita za Saudia zimeshambulia mtaa wa Libbyi mjini Sana'a na kulenga nyumba ya afisa mmoja wa zamani ya jeshi ambaye aliuawa akiwa na mke wake, mwanae wa kiume na watu wengine wa familia hiyo.

Televisheni ya Al Masirah imesema shambulizi hilo lilianza Jumatatu usiku na kuendelea hadi mapema Jumanne. Hilo ni shambulio baya zaidi la muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Sana'a tokea mwaka 2019. Shambulizi hilo limefanyika  baada ya ndege 20 zisizo na rubani pamoja na makombora 10 ya balestiki ya Jeshi na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Yemen kutekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya maeneo muhimu na nyeti ndani ya ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).

Kamanda Mkuu wa majeshi ya Yemen ameionya vikali nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kusisitiza kuwa, kama Abu Dhabi itaendelea kushiriki katika mashambulizi na jinai dhidi ya wananchi wa Yemen, basi wanamapambano wa Yemen watasambaratisha uchumi wa UAE unaotegemea uwekezaji wa kigeni. Jeshi la Yemen pia hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara ya kulipiza kisasi dhidi ya Saudi Arabia.

Moshi ukitanda Abu Dhabi  kufuatia shambulizi la ulipizaji kisasi la Jeshi la Yemen 

Moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen Machi 2015 na kuendelea hadi sasa umeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwalazimisha wengine milioni nne kuwa wakimbizi.

Uchokozi na uvamzi wa kijeshi wa Sadia dhidi ya Yemen umebomoa na kuharibu zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu na kuisababishia pia uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

Tags