Jan 20, 2022 09:35 UTC
  • Safari tarajiwa ya rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Uturuki

Baadhi ya matukio ya miaka ya hivi karibuni yanaonyesha kuwepo mkakati maalumu wa kuanzishwa tena uhusiano wa karibu baina ya Uturuki na utawala wa kibaguzi wa Israel.

Kadhia ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi ni kati ya matukio muhimu ambayo yamejiri katika miaka ya karibuni kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Ni kwa msingi huo ndipo wananchi katika nchi za eneo wakawa na wasiwasi mkubwa kuhusu hatua zinazochukuliwa na tawala zao katika kuanzisha uhusiano na utawala wa kigaidi wa Israel.

Inafaa kuashiria hapa kuwa Uturuki ni moja ya nchi za eneo ambazo ziko mbioni kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Uturuki pia inajaribu kuboresha uhusiano wake ulioharibika na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Uturuki ilizituhumu nchi hizo mbili kuwa ziliusika na jaribio la kuipindua serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan mwaka 2016 na hivyo huo ukawa mwanzo wa kuvurugika uhusiano. Katika miezi ya hivi karibuni wakuu wa Uturuki wamekuwa wakifanya mazungumzo na wakuu wa Saudia na UAE lakini bado mapatano ya kuridhisha hayajaweza kufikiwa.

Issac Herzog, rais wa utawala haramu wa Israel

Inadokezwa kuwa, nchi hizo za Kiarabu zimemfahamisha rais wa Uturuki kuwa sharti la uhusiano kuboreka ni kuwa Uturuki ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala wa kibaguzi wa Israel. Sharti hilo la nchi hizo mbili za Kiarabu linatazamwa na watu wa Uturuki kuwa ni udhalilishaji mkubwa.

Hivi sasa inaelekea kuwa, kutokana na matatizo ya kiuchumi na mashinikizo, wakuu wa Uturuki wanachukua hatua isiyo sahihi ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Ni wazi kuwa wakuu wa Uturuki wanaitazama kadhia ya Palestina kama wanavyoitazama kadhia ya Nagorno-Karabakh. Hivyo ni wazi kuwa Uturuki inaunga mkono masuala muhimu ya Umma wa Kiislamu maadamu uungaji mkono huo unaenda sambamba na maslahi yake ya kitaifa. Katika upande wa pili maadamu suala lolote, hata liwe la Waislamu, haliendi sambamba na maslahi ya Uturuki, basi wakuu wa Ankara hawaliungi mkono.

Kwa miaka kadhaa sasa serikali ya Uturuki imekuwa ikijionyesha kuwa ni muungaji mkono wa Palestina ili iweze kufikia malengo yake ya kisiasa na kijamii. Uturuki pia imekuwa ikifanya hivyo ili kujionyesha kuwa ni nchi muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Hivi sasa kutokana na mgogoro wa kiuchumi, serikali ya Erdogan imeamua kupuuza kadhia ya Palestina na kujikurubisha kwa utawala haramu wa Israel kwa ajili ya maslahi yake ya kitaifa. Ni katika fremu hii  ndio Rais Erdogan akasema kuwa yamkini rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel  Isaac Herzog akaitembelea Ankara. Aidha Erdogan amedokeza kuwa tayari ameshafanya mazungumzo kwa njia ya simu  na Herzog na kusema atatemeblea Uturuki.

Kuhusiana na kadhia hii, televisheni za utawala wa Kizayuni wa Israel Jumatano ziliwanukulu maafisa wa utawala huo wakisema, tayari Erdogan ameshampa Herzog mwaliko rasmi kutembelea Uturuki. Hali kadhalika vyombo vya habari vimeripoti kuwa, Erdogan amependekeza kuwa kujengwe bomba la gesi la kusafrisha gesi kutoka utawala haramu wa Israel hadi Ulaya kupitia Uturuki. Katika kujibu pendekezo hilo wakuu wa utawala wa Kizayuni wamesema: "Mapatano yoyote katika uga huo ambayo yatavuruga uhusiano wa kistratijia baina ya Israel na Ugiriki pamoja na Cyprus, hayakubaliki."

Matamshi ya wakuu wawa utawala haramu wa Israel yanaonyesha wazi kuwa, utawala huo wa Kizayuni hauko tayari kuanzisha uhusiano na Uturuki iwapo hatua hiyo itavuruga uhusiano na waitifaki wake hasa Ugiriki na Cyprus ambao ni mahasimu wa Uturuki.

La kushangaza ni kuwa pamoja na kuwa serikali ya Uturuki inaendelea kudhalilishwa na Israel, wakuu wa nchi hiyo bado wanataka kumpokea rais wa utawala haramu wa Israel.

Tags