Jan 20, 2022 10:37 UTC
  • Nchi nne za Ulaya zataka kusimamishwa ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi nne za Ulaya ambazo ni Ufaransa, Ujerumani, Italia na Hispania wamesema kuwa uamuzi wa viongozi wa utawala haramu wa Israel wa kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, watawala wa Israel walitangaza mpango wa kujenga nyumba mpya karibu 2,500 katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu ambapo karibu nusu ya nyumba hizo zinatazamiwa kujengwa katika maeneo yanayozozaniwa ya "Jiwat Hamatos" and "Har Hama."

Kwa msingi huo taarifa iliyotolewa na nchi nne za Ulaya zilizotajwa imeashiria juhudi nyingi za kimataifa ambazo zimefanywa na pande tofauti kwa ajili ya kutatua kwa amani mzozo wa kunyakuliwa ardhi za Wapalestina pamoja na kubuniwa taifa huru la Palestina na kuongeza kuwa, kujengwa nyumba mpya za walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel bila shaka kutazidisha tu matatizo yaliyopo katika eneo la Asia Magharibi.

Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Kufikia sasa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israe haijatoa tamko lolote kuhusiana na taarifa hiyo ya nchi nne za Ulaya.

Nchi nyingi duniani zimelaani na kukosoa vikali hatua ya ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina na kusisitiza kuwa huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Tags