Jan 21, 2022 03:17 UTC
  • Imarati yaomba msaada wa haraka kwa Wazayuni baada ya kipigo cha operesheni

Imarati imeukimbilia utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuomba msaada wa haraka baada ya operesheni kubwa ya shambulio "Kimbunga cha Yemen" iliyolenga mji wa Abu Dhabi na kusababisha hasara kubwa kwa nchi hiyo ya mali na roho za watu.

Baada ya kupata hasara kubwa kutokana na operesheni kubwa ya "Kimbunga cha Yemen", utawala wa Imarati umeomba msaada wa haraka kwa Wazayuni kwa ajili ya kununua mtambo wa ulinzi wa anga.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, shirika la kizayuni la SKYLOCK linaloshughulika na uundaji wa mitambo ya ulinzi wa anga limetangaza kuwa, Imarati imeliomba shirika hilo msaada wa haraka na imo mbioni kununua mtambo wa makombora kwa utawala haramu wa Israel.

Kabla ya hapo, Sheikh Ali al Asadi, mkuu wa baraza la kisiasa la serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen alipongeza operesheni ya makombora ya ndege zisizo na rubani za vikosi vya Yemen iliyofanywa kujibu uchokozi wa utawala wa Imarati na akasema, "tunawapongeza ndugu zetu Wayemeni kwa ushindi uliopatikana dhidi ya utawala wa Imarati, ambao ni chanzo cha uharibifu na bawa la shari na uistikbari katika eneo."

Imarati inashirikiana kikamilifu na Saudi Arabia katika vita dhidi ya Yemen

Aidha, Sheikh Ali al Asadi amekosoa hatua inazochukua Imarati katika eneo na akabainisha kwamba, nchi hiyo ndogo inapaparika kutaka kujipa nafasi ya kufanya mambo makubwa zaidi ya uwezo wake huku ikijivika vazi ambalo si kadiri ya ukubwa ilionao!

Siku ya Jumatatu jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi vilitekeleza operesheni iliyopewea jina la "Kimbunga cha Yemen" ya mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani ndani ya ardhi ya Imarati, ambayo ilisababisha miripuko karibu na matangi ya shirika kubwa la mafuta la ADNOC na karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abu Dhabi. Watu watatu waliuawa na wengine sita walijeruhiwa katika operesheni hiyo.../