Jan 21, 2022 07:59 UTC
  • Maafisa usalama wanne wa Iraq watiwa mbaroni kwa kuifanyia ujasusi Israel

Duru za habari zimetangaza kuwa, maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa usalama wa ndani wa Iraq wametiwa mbaroni kwa kosa la kuufanyia ujasusi utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shirika la habari la "al Maaluma" limenukuu baadhi ya duru za Iraq zikithibitisha habari hiyo na kusema kuwa, Mahakama Kuu ya Iraq jana Alkhamisi ilitoa amri ya kuwekwa kizuizi maafisa wanne wa ngazi za juu wa shirika la kijasusi la nchi hiyo kwa kufanya njama za kuanzisha kanali maalumu ya kijasusi ya kulitumikia shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD na kushiriki katika operesheni maalumu za majasusi Wazayuni. 

Bendera ya utawala wa Kizayuni

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Meja Jenerali Majid al Dulaimi ambaye ni mtu wa karibu sana na Waziri Mkuu Mustafa al Kadhimi pamoja na Ahmad Abu Raif, kaimu wa al Dulaimi ni miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu wa shirika la kijasusi la Iraq ambao imetoka amri ya kutiwa mbaroni.

Ni vyema kusema hapa kwamba, baada ya kusambaratishwa magenge ya kigaidi nchini Iraq hasa lile la Daesh (ISIS) ambalo ni miongoni mwa magenge ya ukufurishaji yanayoutumikia utawala wa Kizayuni wa Israel na madola ya kibeberu, sasa Tel Aviv imeelekeza nguvu zake katika kujipenyeza ndani ya muundo wa kijeshi na kisiasa wa Iraq ili kuidhoofisha harakati ya kujitolea ya wananchi wa nchi hiyo, al Hashd al Shaabi na taasisi nyingine zenye nguvu nchini humo.