Jan 21, 2022 09:57 UTC
  • Imarati; kujitanua kwenye madhara makubwa

Umoja wa Falme za Kiarabu au kwa jina jingeni Imarati inatekeleza siasa za kujitanua katika eneo la Asia Magharibi, siasa ambazo huenda zikawa na madhara makubwa kwa nchi hiyo.

Katika muongo mmoja uliopita Imarati imeimarisha siasa zake za kujitanua katika eneo la Asia Magharibi. Mwaka 2011 ilishirikiana na nchi wanachama wa shirika la kijeshi la Nato katika kuivamia Libya, Katika mgogoro wa Syria pia nchi hiyo ilishiriki kikamilifu katika njama ya kutaka kuungasha mfumo wa serikali halali ya nchi hiyo iliyoandaliwa na kutekelezwa na wapinzani na makundi ya kigaidi kwa ushirikiano wa nchi za Magharibi. Imatari pia ilishirikiana kwa karibu na Saudia Arabia katika mzingiro ulioanzishwa na nchi hiyo dhidi ya Qatar. Pamoja na hayo kilele cha siasa hizo za kujitanua na uingiliaji za Imarati zilionekana huko Yemen ambapo ilishirikiana kwa karibu na Saudia pia katika vita vya kivamizi na kidhalimu dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Vita vya Yemen vimekuwa na matatizo na madhara mengi. Vita hivyo vimesababisha hasara na maafa makubwa ambayo yameamsha hasira ya jamii ya kimataifa. Licha ya kuwa ni Saudia ndiyo inapasa kulaumiwa kwanza kwa kuanzisha vita hivyo, lakini Imarati nayo pia inapasa kulaumiwa kwa kushirikiana na Saudia katika uvamizi huo. Wakosoaji wa siasa za Imarati wanasema nchi hiyo imeeneza siasa zake hizo za kujitanua kwa kasi kubwa kiasi kwamba madhara ambayo yamesabishwa na siasa hizo ni makubwa kuliko ilivyotarajiwa na watawala wa nchi hiyo. Wanasema hali hiyo imepelekea Imarati kupoteza nafasi na sifa yake ya kuwa nchi tulivu na yenye amani katika eneo.

Ushirikiano mkubwa wa Imarati na nchi za Magharibi na Wazayuni

Mashambulio yaliyofanywa Jumatatu ya tarehe 17 mwezi huu na jeshi pamoja na kamati za wananchi wa Yemen dhidi ya Abu Dhabi, mji mkuu wa Imarati ambayo yalisababisha hasara kubwa ya kiuchumi na kupelekea watu watatu kuuawa na wengine 6 kujeruhiwa, ni dalili inayothibitisha wazi kwamba kiwango cha kudhurika Imarati kutokana na siasa zake za kujitanua katika eneo, ni kikubwa mno. Kiwango hicho cha madhara kinaweza kutathminiwa katika mitazamo miwili.

Wa kwanza ni kuwa Imarati inajaribu kujidhihirisha kuwa eneo na kitovu muhimu cha kiuchumi na kifedha katika eneo la Asia Magharibi na imekuwa ikitekeleza sera maalumu kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Ni wazi kuwa lengo hilo linaweza kufikiwa tu iwapo kutakuwepo na usalama wa uwekezaji na pia usalama wa kijografia na kieneo. Bila shaka siasa za uingiliaji na vita zinazotekelezwa na Imarati dhidi ya nchi nyingine katika eneo zitadhoofisha nchi hiyo na hatimaye kuifanya isiweze kufikia malengo yake.

Mtazamo wa pili ni kwamba wahamiaji wanaunda karibu asilimia 90 ya watu wa Imarati na ndio wanaojenga na kutengeneza miundomsingi muhimu ya nchi hiyo yakiwemo mahospitali na mabarabara, na pia sehemu kubwa ya jeshi la nchi hiyo inaendeshwa na wageni. Kuendelea mashambulio ya Yemen dhidi ya Imarati kunaweza kuwatia wasiwasi wahajiri hao na kuwapelekea waondoke katika nchi hiyo ilihali inawahitajia katika utekelezaji wa miradi yake ya kiuchumi. Ni wazi kuwa matokeo ya hali hiyo yatakuwa na madhara makubwa ya kiuchumi kwa Imarati. Jambo hilo bila shaka litakuwa na taathira kubwa hasi dhidi ya miundomsingi ya nchi hiyo ambayo imepata umashuhuri kutokana na kunawiri uchumi wake katika eneo.

Askari vamizi wa Imarati wakiwa katika kisiwa cha Socotra cha Yemen

Ili kukabiliana na hali hiyo, serilaki ya Imarati imeanza kuwekeza katika miradi ambayo inawanufaisha tu Wazayuni. Televisheni ya al-Jazeera imeripoti kuwa baada ya kupata hasara kubwa iliyosababishwa na mashambulizi ya karibuni ya Yemen, Imarati imeagiza mfumo wa kukabiliana na makombora kutoka utawala haramu wa Israel. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kampuni ya Kizayuni ya "Sky Lock" ambayo inajishughulisha na uzalishaji wa makombora ya ulinzi wa anga, inasema Imarati imeiomba msaada wa haraka katika uwanja huo na kwamba imeamua kununua mfumo wa makombora kutoka kampuni hiyo ya utawala wa Kizayuni.

Pamoja na hayo ni wazi kuwa msaada huo hautailetea Imarati usalama wala utulivu kwa sababu nchi hiyo tayari ni moja ya wanunuzi wakubwa wa silaha za kisasa kutoka nchi za Magharibi na hasa Marekani, lakini haijaweza kujidhaminia usalama kutokana na silaha hizo. Kwa msingi huo ni wazi kuwa kununua mfumo wa makombora kutoka utawala haramu wa Israel hakutaidhaminia Imarati usalama wake bali ni Wazyuni ndio watanufaika zaidi kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na nchi hiyo ya Kiarabu.

 

Tags