Jan 22, 2022 02:38 UTC
  • Mohamed Abdul-Salaam
    Mohamed Abdul-Salaam

Msemaji wa Harakati ya Wananchi ya Ansrullah ya Yemen amesisitiza kuwa, harakati hiyo na wananchi shupavu wa nchi hiyo watatoa majibu makali na kwa nguvu zote dhidi ya madola vamizi yanayoongozwa na utawala wa wa Saudi Arabia.

Mohamed Abdul-Salaam ambaye pia mkuu wa timu ya mazungumzo ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema hayo baada ya makumi ya raia kuuawa kufuatia mashambulio ya anga ya Saudia dhidi ya makazi ya raia katika mji wa bandari wa al-Hudaydah huko Yemen.

Afisa huyo mwandamizi wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesisitiza katika ujumbe wake kwenyye mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Kuwaua wafungwa wa gereza la Sa'dah, raia katika miji ya al-Hudaydah na Sana'a sambamba na kushambuliwa na wavamizi taasisi za kiraia, ni jinai ambazo katu haziwezi kuwafanya wananchi wa Yemen wasalimu amri au irada na azma yao idhoofike.

Aidha ameongeza kuwa, jinai hizi zitazidi kuwafanya wananchi wa Yemen kutoa majibu ya uvamizi huo kwa nguvu zao zote na kutetea haki na ardhi yao.

Ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudi Arabia jana zilishambulia nyumba za watu katika mji wa Magharibi wa Hudaydah na jengo moja la mahabusu kaskazini ya mji wa Sa'dah ambapo zaidi ya watu 180 waliuawa na kujeruhiwa katika jinai hiyo.

Kufuatia shambulio hilo la kinyama la ndege za kivita za Saudi Arabia, dhidi ya maeneo ya raia mjini Hudaydah, Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema, hujuma hiyo ni "jinai ya kivita" na "haisameheki."