Jan 22, 2022 08:04 UTC
  • Brigedia Yahya Saree: Makampuni ya kigeni yanashauriwa kuondoka Imarati

Msemaji wa Jeshi la Yemen ameyashauri makampuni ya kigeni ya uwekezaji kuondoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Yahya Saree, msemaji wa Jeshi la Yemen ametoa taarifa akisema kuwa baada ya ukatili uliofanywa na jeshi la anga la muungano wa Saudia, Marekani na Imarati dhidi ya watu wa Yemen, tunayashauri makampuni kigeni kuondoka katika nchi ndogo ya UAE.

Brigedia Saree amesisitiza kwamba, maadamu watawala wa Imarati wanaendelea na uchokozi wao dhidi ya Yemen, hii itakuwa na maana kwamba makampuni ya kigeni yaliyowekeza katika nchi hiyo ndogo hayatakuwa salama.

Matamshi hayo ya msemaji wa Jeshi la Yemen yametolewa kufutia hujuma kubwa ya ndege za kivita za Saudi Arabia iliyolenga makazi na raia na jela la mkoa wa Sa'ada. Watu wasiopungua 80 wameuawa katika mashambulizi hayo ya kinyama na wengine karibu 150 wamejeruhiwa. 

Kufuatia shambulio hilo la kinyama la ndege za kivita za Saudi Arabia, dhidi ya maeneo ya raia huko Yemen, Muhammad Ali al-Houthi, mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la nchi hiyo amesema, hujuma hiyo ni "jinai ya kivita" na "haisameheki."

Amesema wananchi shupavu wa Yemen watatoa majibu makali na kwa nguvu zote dhidi ya madola vamizi yanayoongozwa na utawala wa wa Saudi Arabia.

Tags