Jan 22, 2022 11:55 UTC
  • Kutiwa nguvuni maafisa wa ngazi za juu wa upelelezi Iraq kwa kufanya ujasusi kwa maslahi ya Mossad

Baadhi ya duru za Iraq zimetangaza kuwa Mahakama Kuu ya nchi hiyo juzi Alhamisi iliagiza kutiwa mbaroni maafisa wanne wa ngazi ya juu wa Idara ya Intelijinsia ya nchi hiyo kwa uhalifu wa kuasisi mtandao wa kijasusi kwa maslahi ya Shirika la Ujasusi la Israel na Kitengo cha Oparesheni Maalumu cha Mossad.

Suala la uhusiano wa Iraq na utawala wa Kizayuni katika miezi ya karibuni limekuwa likifuatiliwa kwa karibu kutokea pande kadhaa. Baada ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni, suala la kuongezeka nchi za Kiarabu kufuata mkondo huo limekuwa likizungumziwa. Wakati huohuo sababu iliyopelekea Iraq kutiliwa maanani kuhusu uhusiano na Israel ni hii kwamba kinyume na nchi nne za Kiarabu zilizoanzisha uhusiano na utawala wa Israel, Iraq ni nchi muhimu na yenye taathira katika eneo hili ambapo makundi ya muqawama pia yapo nchini humo. 

Katika hali ambayo nchi nne za Kiarabu zilizoanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel zilikuwepo katika mhimili wa mapatano na tangu kitambo nyuma zilikuwa na uhusiano wa siri na Israel; Iraq kwa upande wake ni sehemu ya mhimili wa muqawama na wala haijawahi kuwa na uhusiano wa siri na utawala ghasibu unaoikalia Quds kwa mabavu. Ndio maana utawala wa Kizayuni umeliweka katika ajenda yake ya kazi na ya waitifaki wake wa Magharibi khususan Marekani suala la kuiingiza Iraq katika kalibu ya nchi zilizoanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo.   

Eneo la Kurdistan ambalo kimsingi linafanya kila liwezalo ili kujiendeshea mambo yake lenyewe huku mashirika mbalimbali ya Israel pia yakiwepo pakubwa katika eneo hilo; hatua yake ya awali iliyotekeleza ilikuwa ni kuhuisha uhusiano kati ya Iraq na Israel. Kwa mara ya kwanza mwezi Septemba mwaka jana shakhsia wa jamii za jadi wa Iraq walifanya kikao huko Arbil ambapo walizungumzia suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Iraq na Israel. Hata hivyo wananchi wa Iraq walionyesha radiamali yao kufuatia kikao hicho na kueleza kuwa Iraq si mahala rahisi pa kufanikisha mpango wa kuanzisha uhusiano rasmi na Israel. Viongozi rasmi wa Iraq pia walionyesha radiamali yao kwa kikao hicho cha Arbil. Rais Barhum Salih wa Iraq alisisitiza katika taarifa aliyoitoa juu ya msimamo thabiti wa nchi hiyo wa kuiunga mkono kadhia ya Palestina na kupatikana haki halali na kamili za wananchi wa Palestina. Aidha alibainisha kuwa, Iraq inapinga vikali kuanzisha uhusiano rasmi na Israel. Kikao kilichofanyika hivi karibuni kwa lengo la kueneza suala hilo hakijaakisi mtazamo wa wananchi wa Iraq bali kinadhihirisha mtazamo wa washiriki wa kikao hicho. 

Eneo la Kurdistan nchini Iraq 

Hata kama inawezekana suala la kufanyika ujasusi kwa maslahi ya utawala wa Kzayuni lilikuwepo pia Iraq kabla ya kuibuka kadhia hii ya karibuni lakini pande zinazounga mkono suala la kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Kizayuni zimeliweka katika ajenda yao ya kazi suala la kujipenyeza katika Idara ya Intelijinsia ya Iraq. Kuhusiana na suala hilo, vyombo mbalimbali vya habari  vimetangaza kuwa maafisa kadhaa wa ngazi za juu katika Idara ya Intelijinsia ya Iraq wametiwa nguvuni kwa kosa la kufanya ujasusi kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni; ambapo miongoni mwa waliotiwa nguvuni ni pamoja na Meja Jenerali Majid al Dulaimi Mkurugenzi wa Idara ya Intelijinsia ya Iraq ambaye anatajwa kuwa shakhsia wa karibu sana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mustafa al Kadhimi na vilevile Ahmad Abu Raghif Naibu Mkuu wa Idara ya Intelijinsia ya Iraq. Kwa mujibu wa ripoti ya maafisa wa Idara ya Intelijinsia ya Iraq na kwa mujibu wa watu waliohojiwa, Mossad ilikuwa tayari imeasisi mtandao ndani ya Idara ya Intelijinsia ya Iraq.   

Hata kama kutiwa nguvuni watu hao ni pigo la kiitelijinsia kwa waungaji mkono wa suala la kuanzisha uhusiano rasmi baina ya Iraq na Israel lakini imedhhirika wazi kuwa utawala wa Kizayuni ulikuwa umepanga mkakati maalumu la kuibua mgawanyiko ndani ya mfumo wa uongozi wa Iraq kuhusu kadhia hiyo. Pamoja na hayo utawala wa Kizayuni na pande zinazouunga mkono na kuukingia kifua utawala huo haramu huko Iraq zimekumbana na kizuizi kikuu kwa jina la muqawama na idadi kubwa ya wananchi ambao wanapinga kwa nguvu zao zote nchi yao kuanzisha uhusiano rasmi na Israel. Hadi al A'miri Mkuu wa  Muungano wa al-Fat'h katika Bunge la Iraq aliwahi kusema kuwa: 'Muungano na wanamuqawama wa Iraq watasimama imara na kukabiliana kwa nguvu zote na njama za kuuunga mkono kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.'

Hadi al A'miri, Mkuu wa  Muungano wa al-Fat'h katika Bunge la Iraq

 

Tags