Jan 23, 2022 12:20 UTC
  • UNICEF: Kwa akali watoto 17 wameuawa nchini Yemen tangu kuanza mwezi huu wa Januari

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, kwa akali watoto 17 wameuawa nchini Yemen tangu kuanza mwezi huu wa Januari kufuatia mashambulio ya anga ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Ted Chaiban, Mkurugenzi wa UNICEF katika Kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika ametangaza kuwa, tangu kuanza kwa mwezi huu wa Januari watoto wapatao 17 wameuawa nchini Yemen, idadi ambayo ni mara mbili ya watoto wote waliouawa nchini humo katika mwezi uuliopita wa Disemba.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) amebainisha kuwa, watoto wa Yemen wameendelea kuwa wahanga wa kwanza walnaolipa gharama ya vita vya Yemen vinavyoendelea kwa mwaka wa saba sasa.

Chaiban amezitaka pande zote nchini Yemen kufanya kila ziwezalo kuwalinda watoto sambamba na kujiepusha kushambulia makazi ya raia pamoja na miundombinu ya nchi hiyo iliyoharibiwa vibaya na vita vya Saudia na washirika wake.

Wananchi wa Yemen wakichimba makaburi ili kuwazika wapendwa wao waliouawa na mashambulio ya Saudia na washirikka wake.

 

Katika upande mwingine, mamia ya watoto wa Yemen wanafariki dunia ndani ya kila saa 24 kutokana na utapiamlo, huku muungano wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia ukiendelea kufanya mashambulizi na kuliwewekea mzingiro wa kila upande taifa hilo maskini la Kiarabu.

Kufuatia uungaji mkono wa Marekani, Imarati, utawala haramu wa Israel na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu, Saudi Arabia iliivamia kijeshi nchi masikini ya Yemen mnamo Machi 2015 na kuiwekea mzingiro wa pande zote wa nchi kavu, anga na majini. Uvamizi wa kijeshi wa Saudia umeisababishia pia nchi masikini ya Yemen uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

Tags