Jan 25, 2022 02:29 UTC
  • Mufti wa Lebanon: Moto wa vita vya Yemen utachoma miji mikuu ya nchi za Kiarabu

Mufti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Lebanon amesema kuwa, iwapo moto wa vita vya Yemen hautazimwa, utachoma pia miji mikuu ya nchi za Kiarabu.

Sheikh Ahmed Qabalan ambaye alikuwa akizungumzia mapigano yaliyopamba moto zaidi huko Yemen ameziambia serikali za nchi za Kiarabu kwamba: "Zimeni moto wa Yemen kabla ya miji mikuu ya Waarabu haijateketea kwa moto."

Kiongozi huyo wa kidini wa Lebanon amesisitiza kuwa, viongozi wa nchi za Kiarabu wanaelewa vyema kwamba Yemen ina nguvu kubwa kiasi kwamba haiwezi kushindwa na kuongeza kuwa, yanayotokea huko Yemen ni vita vya kiwendawazimu na haramu ambavyo vinaufaidisha tu utawala haramu wa Israel na Marekani.

Ndege za muungano wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia zimezidisha mashambulizi makali dhidi ya miji ya Sana'a, al-Hudaydah na Sa'ada nchini Yemen tangu Jumanne iliyopita baada ya ndege zisizo na rubani na makombora ya kulipiza kisasi ya jeshi na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah nchini Yemen, kulenga maeneo muhimu katika mji mkuu wa Imarati, Abu Dhabi.

Ijumaa iliyopita pekee, muungano huo wa nchi vamizi zikiongozwa na Saudi ulishambulia Sa'ada, Yemen, na kuua watu 87. Wengine 266 walijeruhiwa. 

Tags