Jan 26, 2022 04:12 UTC
  • Kupoteza hadhi Jumuiya ya Nchi za Kiarabu baada ya kukengeuka njia na malengo ya kuasisiwa kwake

Utambulisho na jukumu la uwepo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ni kuunga mkono mataifa ya Kiarabu na kutatua matatizo na migogoro inayozikabili nchi hizo.

Matukio ya miaka ya hivi karibuni yaliyojiri katika mataifa ya Kiarabu hususan kuanzia mwaka 2011, kivitendo yamethibitisha bayana kutokuwa na faida yoyote uwepo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kukosa maana na hadhi ya uwepo wake. Matukio ya miaka ya hivi karibuni katika nchi kama Iraq, Syria, Palestina, Lebanon, Sudan, Libya, Algeria na Morocco ni ushahidi tosha na wa wazi kabisa wa madai haya, matukio ambayo yameifanya jumuiya hiyo kupoteza maana yake baada ya kugeuzwa na kuwa mwanasere wa Saudi Arabia.

Kwa karibu miaka 7 sasa ambapo Yemen imekuwa ikiandamwa na hujuma na mashambulio ya kinyama ya muungano wa Saudia-Imarati ambapo katika miaka yote hii Jumuiya ya Nchi za Kiarabu siyo tu kwamba haijawa nafasi yoyote ile ya maana katika kuipatia ufumbuzi migogoro ya nchi wanachama, bali misimamo yake imekuwa katika mkondo wa kusukuma mbele gurudumu la siasa za wavamizi dhidi ya Yemen. Jumapili iliyopita na katika msimamo wa karibuni kabisa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliitisha kikao cha dharura kwa ombi la Imarati kikao ambacho kilihudhuriwa na wawakilishi wa kudumu wa jumuiya hiyo.

Kikao hicho kiliitishwa kwa ajili ya kujadili mashambulio ya hivi karibuni ya Jeshi la Yemen dhidi ya mji mkuu wa Imarati Abu Dhabi, mashambulio ambayo yalitetekelezwa kwa ajili ya kujibu jinai za Imarati dhidi ya wananchi wa Yemen.

Mashambulio ya Wayamen dhidi ya Abu Dhabi

 

Aidha kikao hicho kiliitishwa kwa minajili ya kuchukua maamuzi kuhusiana na kikao kijacho cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi wanachama dhidi ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ili natija yake iwe ni kuitaka Marekani na mataifa ya Kiarabu waiweke Ansarullah ya Yemen katika orodha inayojulikana kama ya makundi ya kigaidi.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imetoa radiamali yake kuhusiana na kikao hicho cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kusisitiza kwamba, taarifa ya jumuiya hiyo ya kuwalaani Wayamen haina maana na haiakisi dhamira za Waarabu na msimamo wa fikra za waliowengi katika mataifa ya Kiarabu na kimsingi jumuiya hiyo imekufa zaidi ya miaka 40 katika dhamira za wananchi wa mataifa haya na hii leo imetengwa kikamilifu.

Baada ya operesheni ya kijeshi ya hivi karibuni ya mashambulio ya droni ya Jeshi la Yemen na Kamati za Wananchi wa Yemen dhidi ya mji wa Abu Dhabi, tawala za Imarati na Saudi Arabia zimeshadidisha hujuma na mashambulio yao dhidi ya wananchi wa Yemen, kiasi kwamba, katika operesheni kadhaa za kinyama za vikosi vamizi, makumi ya raia wa Yemen wakiwemo watoto na wanawake wameuawa. Hujuma hiyo ilikuwa kubwa kiasi kwamba, katika kipindi cha saa 24, kulifanyika mashambulio ya anga mara 45 katika maeneo mbalimbali ya Yemen.

Kimsingi ni kuwa, kuna nukta kadhaa za kuashiria kuhusiana na hatua hiyo ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pamoja na nchi wanachama wa jumuuiya hiyo.

 

Nukta ya Kwanza ni kuwa, vyombo vya habari vya Saudia kama Kanali ya Televisheni ya al-Arabiya ikiwa na lengo la kuhalalisha hujuma na mashambulio ya kinyama ya utawala wa Aal Saud na Imarati dhidi ya makazi ya raia na wananchi wasio na ulinzi wa Yemen na uwezekano wa kuendelea mashambulio hayo katika siku za usoni katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, iliakisi kikao hicho kwa mapana na marefu. Mbali na hivyo, kanali hiyo ikitumia ujanja na mbinu maalumu za vita vya kisaikolojia ilifanya njama ya kuionyesha Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen na Ansarullah ya Yemen kwamba, hazina itibari na kwa msingi huo ikapindua mambo juu chini kwa kuonyesha mvamizi ndiye muhanga ilihali wananchi wa Yemern ndio wahanga wa vita na hujuma hiyo.

Nukta ya Pili; ni kwamba, muungano vamizi wa Saudi-Imarati umenasa katika kinamasi katika hujuma na mashambulio yao ya takribani miaka 7 dhidi ya Yemen na hivi sasa umo mbioni kulifanya suala hilo kuwa la wote na hivyo kuyaingiza mataifa mengine ya Kiarabu na Kimagharibi katika kadhia ya Yemen na kwa msingi huo kujiandalia uwanja wa kuondoka kwa heshima katika kinamasi cha Yemen.

Moja ya vikao vya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

 

Nukta ya Tatu; ni kuwa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imepoteza utendaji na maana ya uwepo wake. Hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ya kuitisha kikao hicho, imekuwa sababu ya kupanuka wigo wa hujuma na mashambulio ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen. Kwa muktadha huo, kikao cha asasi kama hii isiyo na irada na azma siyo tu kwamba, hakina maslahi na wananchi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu bali lengo lake ni kufunika uvamizi na njama za wavamizi hao.

Nukta ya Nne; kuhusiana na kadhia hii ni kwamba, hatua ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ya kufanya kikao kama hiki kimsingi lengo lake ni kutaka watu wasahau masuala ya kimsingi na makuu ya wananchi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu; kwani badala ya kujikita katika masuala ya kimsingi ya Ulimwengu wa Kiislamu kama kadhia ya Palestina ambapo matatizo na migogoro mbalimbali inapaswa kupatiwa ufumbuzi ndani ya mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, imekuwa ikifanya mambo kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumuu la malengo ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani na hivyo kukengeuka kikamilifu njia na malengo ya kuasisiwa jumuiya hiyo.