Jan 26, 2022 12:15 UTC
  • Rais wa utawala haramu wa Israel kuitembelea Imarati

Rais wa utawala haramu wa Israel anatazamiwa kufanya safari ya kwanza ya kuutembelea Umoja wa Falme za Kiarabu wiki ijayo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, Isaac Herzog anatazamiwa kuelekea Imarati Jumapili ijayo, ambapo amepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Abu Dhabi.

Taarifa ya ofisi ya rais wa utawala ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina imesema, safari ya Herzog nchini Imarati inanuia eti kulibadilisha eneo zima la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi).

Mwezi uliopita, Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni aliitembelea UAE pia, katika safari ya kwanza ya afisa wa ngazi ya juu wa Tel Aviv kuizuru nchi hiyo ya Kiarabu, tangu tawala mbili hizo zianzishe uhusiano wa kawaida.

Maandamano ya kupinga uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida na Israel

Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo Septemba mwaka 2020 ilianzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu kuchukua hatua hiyo ya kisaliti baada ya kipindi cha miaka 26.

Baadhi ya tawala za Kiarabu kama Sudan, Bahrain na Morocco zilifuata mkumbo huo kibubusa, licha ya wananchi katika nchi hizo kufanya maandamano ya kupinga na kulaani uafriti huo.

Tags