Jan 27, 2022 02:36 UTC
  • Israel yatiwa hofu na onyo la Yemen la kushambulia Expo Dubai sambamba na safari ya Herzog UAE

Duru za habari za lugha ya Kiebrania zimeripoti kuwa, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umeingiwa na wasiwasi mkubwa kutokana na onyo lililotolewa na vikosi vya ulinzi vya Yemen la kushambulia maonyesho ya Expo Dubai, sambamba na kukaribia safari ya rais wa utawala huo nchini Imarati.

Televisheni ya al-Mayadeen imezinukuu duru hizo za habari zikifichua kwamba, baada ya mashambulio ya karibuni ya Yemen dhidi ya Imarati na onyo ililotoa Sana'a la uwezekano wa kushambulia maonyesho ya Expo Dubai, viongozi wa utawala wa Kizayuni wamezidi kupatwa na wasiwasi kuhusiana na vitisho na onyo hilo la Yemen na hasa ikitiliwa maanani kuwa, rais wa utawala haramu wa Israel Isaac Herzog anatazamiwa kuelekea Imarati  na kutembelea maonyesho hayo.

Gazeti la Haaretz limeandika, onyo hili limetolewa katika kipindi ambapo Israel na Imarati zimo mbioni kuimarisha zaidi uhusiano wao baada ya kusaini makubaliano ya kuanzisha rasmi uhusiano baina ya pande mbili.

Gazeti hilo la Kiebrania limeongeza kuwa, mbali na masafa ya kilomita elfu mbili, baadhi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya cruise ya Yemen yana uwezo wa kufika hadi eneo la Eilat, Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kombora ya wapiganaji wa Ansarullah wa Yemen

Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, siku ya Jumatatu iliyopita lilitangaza kuwa, operesheni ya "Kimbunga cha Yemen 2" ni mwanzo na utangulizi wa mashambulio yajayo na likasisitiza kuwam vikosi vyake vya ulinza vitafanya mashambulio makali zaidi dhidi ya Imarati na Saudi Arabia.

Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, vikosi vya jeshi la Yemen na vya wapiganaji wa kujitolea wa wananchi, vilitekeleza operesheni mbili za "Kimbunga cha Yemen 1" na "Kimbunga cha Yemen 2" kwa kuishambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani miji ya Abu Dhabi na Dubai ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati.../

Tags