Jan 27, 2022 07:46 UTC
  • Kombora la Yemen laua makumi ya mamluki wa Saudia

Makumi ya mamluki wa muungano vamizi wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia wameangamizwa baada ya vikosi vya jeshi la Yemen kuwavurumishia kombora la balestiki lililopiga kambi ya mamkuli hao katika mkoa wa Ma'rib, katikati mwa Yemen.

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema kombora hilo limelenga mkusanyiko wa mamluki wa serikali iliyojiuzulu ya Abdu Rabbu Mansour Hadi katika maficho yao yanayofahamika kama 'eneo la tatu la kijeshi' mkoani Ma'rib, na kuua kadhaa miongoni mwao, na kujeruhi wengine wengi.

Jenerali Saree amesema kombora hilo limepiga kwa usahihi mkubwa eneo palipokusudiwa, na kuangamiza na kujeruhi makumi miongoni mwa mamluki, likiwa ni shambulio la ulipizaji kisasi.

Mamluki wa Saudia

Haya yanajiri masaa machache baada ya televisheni ya al-Masirah kuripoti kuwa, muungano wa Saudia umefanya hujuma tisa za anga katika wilaya ya al-Jubah mkoani Ma'rib. Hakuna ripoti iiyotolewa kuhusu uharibifu na idadi ya wahanga wa mashambulio hayo.

Muungano vamizi wa Saudia katika siku za hivi karibuni umeshadidisha mashambulizi yake dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen, huku ukipuuza onyo la maafisa wa Sanaa kwa tawala za Saudi Arabia na Imarati zinazozikalia kwa mabavu ardhi ya Yemen.