Jan 28, 2022 05:25 UTC
  • Kuongezeka kwa harakati za pembetatu za Saudia, UAE na utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen

Shambulizi lililofanywa hivi majuzi la makombora na ndege zisizo na rubani za jeshi la Yemen na harakati ya Ansarullah dhidi ya Imarati limeonyesha kuwa harakati za pembetatu ya Saudi Arabia, Imarati na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Yemen zimeongezeka.

Shambulizi hilo lilifanyika kujibu jinai na uhalifu unaoendelea kufanywa na Saudia Arabia na washirika wake huko Yemen.

Vita vya muungano wa shari wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen viliingia mwezi wa 83 juzi Januari 26. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ilitazamiwa kwamba, vita dhidi ya Yemen vitaendelea kwa kasi ndogo, na kwamba pande hizo mbili zitahamia kwenye meza ya mazungumzo na kupunguza mgogoro huo, hasa kwa vile hakuna upande wowote wenye uwezo kamili wa kuushinda upande mwingine. Hata hivyo, wiki hizi za mwanzoni mwa 2022 zimeonyesha kuwa mapigano na mzozo wa Yemen umeongezeka na bado unaendelea kupamba moto. Waimarati wametuma meli iliyokuwa imebeba silaha kwenda Yemen, ambayo ilitekwa na Wayemeni; na katika upande mwingine Wayemeni wameshambulia mji wa Abu Dhabi kwa makombora na ndege za kivita zisizo na rubani. Wasaudia nao ambao walikuwa tayari wamechochea zaidi moto wa vita dhidi ya Yemen kabla ya mashambulizi hayo, wanaendelea kushambulia kwa mabomu maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakilenga makazi ya raia na kuua watu wasio na hatia.

Maeneo ya makazi ya raia katika mkoa wa Sana'a ndiyo yanalengwa zaidi kwa mashambulizi makali ya anga ya ndege za kivita za Saudia. Jumanne iliyopita ndege za kivita za Saudia zililenga mkoa wa kaskazini mwa Yemen wa Sa'ada na kuua watu 91. Watu wengine wasiopungua 236 walijeruhiwa. Waziri wa Afya wa Yemen Al-Mutawakil amesema muungano wa vita unaoongozwa na Saudia unalenga waziwazi raia wasio na hatia na kuwaua kwa makusudi. 

Saudia inaendelea kuua raia waso na hatia wa Yemen

Sambamba na hayo Wazayuni wa Israel pia wamezidisha ushiriki wao katika vita vya Yemen na kuunda muungano wa pande tatu za shari, yaani Israel, Imarati na Saudi Arabia dhidi ya taifa la Waislamu wa Yemen. Utawala wa Kizayuni wa Israel unashiriki kwenye vita hivyo kwa malengo maalumu. Kwa upande mmoja, utawala huo unajaribu kulinda maslahi yake ya kiuchumi kupitia vita vya Yemen, hasa kutoka Imarati (UAE). Kuhusiana na suala hilo, kampuni ya Kizayuni ya "Skylock", inayojishughulisha na uzalishaji wa zana za ulinzi wa anga, imetangaza kuwa, Imarati imeomba msaada wa haraka kutoka kwa kampuni hiyo na inaazimia kununua mfumo wa makombora kutoka kwa utawala wa Kizayuni.

Katika upande mwingine, utawala wa Kizayuni unajaribu kuishawishi Saudi Arabia iweke wazi uhusiano wake na Tel Aviv kwa kuzisaidia Saudia na Imarati katika vita dhidi ya Yemen. Vilevile inataka kuishukuru Abu Dhabi kwa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo khabithi unaoendelea kuua watu wa Palestina na kukalia kwa mabavu kibla cha kwanza cha Waislamu. Ripoti nyingi za kiintelijensia zinaonyesha kuwa, uhusiano wa siri kati ya Riyadh na Tel Aviv umeongezeka sana licha ya kwamba watawala wa kifalme wa Riyadh haujawa tayari kutangaza waziwazi uhusiano huo kutokana na wasiwasi wa matokeo yake mabaya kwa sura ya Saudia katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo, kwa kuzidisha ushiriki wake katika vita dhidi ya Yemen, utawala wa Kizayuni wa Israel unajaribu kuishawishi Saudi Arabia ili ijiunge katika orodha ya nchi za Kiarabu zilizowasaliti Waislamu hususan Wapalestina na kuweka wazi uhusiano wao na utawala huo ghasibu. 

Waimarati wanaendelea kujikomba kwa Wazayuni

Jambo la msingi ni kwamba ijapokuwa ongezeko la mashambulizi ya pembe tatu za Riyadh, Abu Dhabi na Tel Aviv dhidi ya taifa la Yemen litaisababishia nchi hiyo uharibifu wa hali na mali na maafa makubwa ya kuuliwa raia wasio na hatia, lakini halitapelekea kushindwa kwa Wayemeni. Hatua hizo ambazo zimeshuhudiwa mara nyingi katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, kamwe hazitakuwa na matokeo yanayotarajiwa na watawala wa Saudia, Imarati na utawala wa Kizayuni, bali zitazidisha migogoro, mauaji ya raia na fedheha zaidi kwa Wasaudi na waungaji mkono wao Wazayuni na Magharibi katika vita dhidi ya Yemen. 

Kimya cha taasisi za kimataifa na mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu mbele ya jinai na uhalifu wa pembe hizo tatu pia kina taathira kubwa katika maafa na hali mbaya ya sasa huko Yemen.