Jan 28, 2022 10:31 UTC
  • Syria: Silaha za nyuklia za Israel zinatishia amani magharibi mwa Asia

Mwakilishi wa Syria katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amezitaja silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni tishio kubwa kwa usalama na amani katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Syria (SANA), Hussam al-Din Ala, mwakilishi wa Syria katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, amesema kuwa eneo la Asia Magharibi linapaswa kusafishwa na silaha za nyuklia na za maangamizi na kuongeza kuwa ushirikiano wa kimataifa unahitajika kwa ajili ya kukabiliana na hatari zinazotishia dunia.

Ameongeza kuwa, suala hili linaonesha kuwa, jamii ya kimataifa imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kuanzisha eneo lisilo na silaha za nyuklia na za mauaji ya halaiki Magharibi mwa Asia na vilevile katika kuchukua hatua za kivitendo za kuhakikisha utawala wa Kizayuni unajiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, NPT. Amesisitiza kuwa utawala wa kizayuni wa Israel unapaswa kujiunga na mkataba huo bila masharti.

Hussam al-Din Ala

Utawala wa Kizayuni wa Israel ndio utawala pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika eneo la Magharibi mwa Asia na umekataa kutia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) licha ya mashinikizo ya kimataifa.

Tags