Jan 29, 2022 03:00 UTC
  • Wapalestina 25,000 wamesali Sala ya Ijumaa Msikiti wa Al Aqsa katika hali ya baridi kali

Wapalestina wasiopungua 25,000 wamestahamili baridi kali na kushiriki katika Sala ya Ijumaa wiki hii katika Msikiti wa Al Aqsa ulioko katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Palestina, pamoja na kuwa wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel walikuwa wameweka sheria kali za kuwazuia Wapalestina, lakini maelfu walifanikiwa kufika katika msikiti huo mtakatifu kwa ajili ya Sala ya Ijumaa.

Idara ya Wakfu wa Kiislamu Quds imetangaza kuwa Wapalestina wameshiriki katika Sala ya Ijumaa wiki hii.

Wiki hii mji wa Quds umekumbwa na baridi kali ambapo maeneo yote ya msikiti huo yalikuwa yamejaa theluji jambo ambalo liliwaletea furaha tele Wapalestina katika mji huo.

Wapalestina wakifurahia theluji katika pembizoni mwa Qubbat aṣ-Ṣakhra karibu la Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds

Askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel huwazuia Wapalestina wengi kufika katika Msikiti wa Al Aqsa wakati wa Sala ya Ijumaa.

Msikiti wa Al Aqsa umegeuzwa kuwa eneo la kutamba na kujifaragua askari wa utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni wanaochukua hatua zinazolenga kuubadilisha utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa mji wa Quds (Jerusalem) na badala yake kuufanya kuwa na nembo za Uzayuni.

Mji wa Quds ulipo msikiti wa Al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Palestina na moja ya maeneo matatu muhimu zaidi matakatifu ya Kiislamu.