Jan 29, 2022 11:37 UTC
  • Abdallah Bou Habib
    Abdallah Bou Habib

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Lebanon amesema kuwa nchi hiyo haitakabidhi silaha za Hizbullah. Abdallah Bou Habib ameyasema hayo kabla ya mkutano na mawaziri wenzake wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi huko Kuwait unaolenga kuboresha uhusiano.

"Siendi Kuwait kukabidhi silaha za Hizbullah wala sitakomesha uwepo wa Hizbullah; suala hili halina mjadala nchini Lebanon", amesisitiza waziri Bou Habib na kuongeza kuwa, anaenda Kuwait kwa ajili ya mazungumzo. 

Lebanon inashiriki katika mkutano huo wa Jumamosi ya leo ili kujibu masharti ya kuboresha uhusiano ulioharibika wa nchi hiyo na baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kuimarika nguvu za harakati ya Hizbullah katika kanda ya Asia Magharibi. 

Saudi Arabia na washirika wake hususan Imarati wanaituhumu harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuwa inawasaidia wapiganaji wa harakati ya Ansarullah nchini Yemen ambao wanapambana na madola yaliyovamia nchi yao.  

Mapema mwezi huu wa Januari, kiongozi wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah, aliishutumu Riyadh kuwa inaeneza itikadi na misimamo mikali.

Sayyid Hassan Nasrullah

Vilevile harakati hiyo inaulaumu utawala wa kifalme wa Saudi Arabia kwa kumwaga damu za Waislamu wasio na hatia wa Yemen.

Hizbullah ni moja ya wachezaji wakuu na wenye taathira kubwa katika kambi ya mapambano dhidi ya madola ya kibeberu na washirika wao kama Saudi Arabia na Imarati. Saudi Arabia inaona kuwa, nafasi na mafanikio haya ya Hizbullah yanakinzana na maslahi yake na mabwana zake na ndio maana inafanya njama dhidi ya harakati hiyo.

Tags