Feb 01, 2022 03:03 UTC
  • HAMAS: Hatuwezi kukubali kuwa na utulivu wa kiuchumi na Wazayuni wakati bado wamezikalia kwa mabavu ardhi zetu

Kiongozi mmoja wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, harakati hiyo haiwezi kukubali kuwa na usalama wa kiuchumi na utawala wa Kizayuni wa Israel maadamu utawala huo pandikizi unaendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Gazeti la al Ayyam liliripoti habari hiyo jana (Jumatatu) na kumnukuu Suhail al Hindi akisema kuwa, HAMAS haiwezi kukubaliana na masharti ya kiuchumi ya utawala wa Kizayuni maadamu utawala huo unaendelea na jinai zake na bado umezikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Utawala wa Kizayuni umeyaomba makundi ya muqawama ya Palestina ikiwemo HAMAS yasiyashambulie makazi ya Wazayuni na badala yake Israel itapunguza makali ya kuuzingira Ukanda wa Ghaza, lakini Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imekataa kabisa pendekezo hilo.

Bendera ya utawala wa Kizayuni

 

Kiongozi huyo wa HAMAS amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni hauaminiki hata kidogo na kwamba pendekezo lake hilo pia ni la kidanganyifu na la kupoteza wakati. Hakuna ahadi na mkataba wowote unaoheshimiwa na utawala wa Kizayuni.

Amesema, kama utawala wa Kizayuni unataka kweli usalama wake, basi usikilize matakwa ya muqawama wa Palestina na uache kabisa kuuzingira Ukanda wa Ghaza, la sivyo, hakuna dhamana yoyote ya kubakia salama makazi ya walowezi wa Kizayuni.

Kiongozi huyo wa HAMAS aidha ametoa onyo kwa utawala wa Kizayuni kwamba kipimo cha usalama wake ni kutoizingira Ghaza na huenda kupunguzwa makali ya mzingiro huo yakapelekea kupungua hali ya wasiwasi. 

Tags