Feb 02, 2022 02:34 UTC
  • Hamas yapongeza ripoti ya Amnesty International inayoitaja Israel kuwa ni

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepongeza ripoti ya Amnesty International iliyochapishwa jana Jumanne ambayo imeitambua Israel kuwa ni utawala wa kibaguzi wa apartheid.

Mkuu wa idara ya Habari ya Hamas, Hisham Kassem amesema - katika taarifa yake - kwamba harakati hiyo inapongeza kwa kuheshimu juhudi za Amnesty International katika kutoa ripoti yake ya kitaalamu ambayo imezingatia ukweli na uhakika wa mambo.

Kassem amesema kwamba ripoti hiyo inaeleza hali halisi ya kusikitisha ya watu wa Palestina wanaokaliwa kwa mabavu, kwa kuutambua utawala ghasibu wa Israel kuwa ni utawala wa kibaguzi unaotekeleza mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid katika ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Taarifa hiyo ya Hamas pia imeitaja ripoti ya Amnesty International kuwa inatoa "mchango mpya katika kufichua uvamizi wa Israel na kuondoa pazia linaloficha uhalifu mkubwa wa utawala huo kwa miongo kadhaa, iwe ni kupitia madola makubwa ya kikoloni au kwa kufumbiwa macho na taasisi za kimataifa."

Athari za mashambulizi ya Israel Ukanda wa Gaza

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa kampeni ya Israel dhidi ya Amnesty International – baada ya kutolewa ripoti hiyo - ni juhudi nyingine zinazoongezwa kwenye ubaguzi wa kinyama wa uvamizi wa utawala huo, za kutaka kuicha ukweli mbele macho ya walimwengu.

Ripoti iliyotolewa jana na Amnesty International ilisema kuwa, utawala haramu wa Israel unatumia mbinu za apartheid kuwakandamiza na kuwatesa Wapalestina, sanjari na kukanyaga haki zao za msingi.

Tags