Feb 14, 2022 10:55 UTC

Mapema leo Jumatatu asubuhi, wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wamevamia nyumba moja ya raia wa Kipalestina katika mji wa Jenin wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuua shahidi kijana mmoja wa Kipalestina na kujeruhi wengine 10. Wanajeshi hao makatili wameripua kwa mabomu pia nyumba ya raia mmoja wa Kipalestina.

Televisheni ya al Alam imeweka mkanda wa video katika tovuti yake inayoonesha Wazayuni waliporipua nyumba hiyo ya Mpalestina katika kitongoji cha al Sila al Harithiyyah mjini Jenin.

Televisheni hiyo imeripoti kuwa, wanajeshi Wazayuni wamekivamia kitongoji hicho wakiwa na makumi ya magari ya kijeshi. Vijana mashujaa wa Kipalestina wamesimama kidete kupambana na wanajeshi hao vamizi. Wanajeshi Wazayuni wamewashambulia kwa risasi za kivita vijana hao wa Kipalestina.

Kijana wa miaka 17 wa Kipalestina anayejulikana kwa jina la Akram Ali Tahir Abu Sallah ameuliwa shahidi na wanajeshi hao makatili wa Israel. Wapalestina wengine 10 wamejeruhiwa kwa risasi za kivita za wanajeshi hao wa Israel.

Wanajeshi wakimkandamiza mtoto wa Kipalestina

 

Mkuu wa kitendo cha matibabu ya dharura cha Hospitali Kuu ya Jenin amesisitiza kuwa, wanajeshi Wazayuni wamezuia magari ya wagonjwa kuingia kwenye eneo hilo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa na kuwapeleka hospitalini.

Jana usiku kundi kubwa la wanajeshi wa Israel wakiwa wamejizatiti kwa makumi ya magari ya deraya walilivamia eneo hilo kwa lengo la kuvunja nyumba ya Mpalestina Mahmoud Ghalib Jardat, lakini vijana wa Kipalestina walipamamba nao na kulizuka machafuko makubwa. 

Jana usiku wanajeshi hao vamizi wa utawala wa Kizayuni walishindwa kuifikia nyumba ya Mpalestina huyo. Hata hivyo mapema leo asubuhi wameiripua na kuivunja nyumba ya raia huyo wa Kipalestina.