Feb 18, 2022 03:06 UTC
  • Saudia yarefusha kifungo cha mwanachuoni mashuhuri wa upinzani nchini humo

Mamlaka za Saudi Arabia zimerefusha kifungo cha msomi mashuhuri na mpinzani mkuu wa utawala wa Aal-Saud kwa miaka 8 zaidi, huku ufalme huo ukishadidisha ukandamizaji wa jamii za waliowachache nchini humo.

Shirika la kutetea haki za wafungwa wa itikadi la Prisoners of Conscience limeripoti hayo na kuongeza kuwa, Mahakama ya Rufaa mjini Riyadh imeagiza Sheikh Khalid al-Rashid atumikie kifungo kingine cha miaka minane gerezani, kwa maana kuwa sasa mwanaharakati huyo wa upinzani atafungwa jumla ya miaka 23 jela.

Haya yanajiri licha ya wasimamizi wa gereza lenye ulinzi mkali la Ha'ir lililoko yapata kilomita 40 kusini mwa Riyadh kusema kuwa hali ya kiafya ya mwanachuoni huyo ni mbaya.

Sheikh Rashid alipaswa kuachiwa huru Septemba mwaka 2020 baada ya kutumikia kifungo cha miaka 15 jela. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani hatua ya kuendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria mwanaharakati huyo.

Baadhi ya wanazuoni waliofungwa na walawata wa Aal-Saud

Utawala wa Aal-Saud umewakamata na kuwanyonga makumi ya wanaharakati wa upinzani hususan katika mji wa Qatif, Mkoa wa Mashariki ambao aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za wafungwa wa itikadi la Prisoners of Conscience, wanaharakati 2,613 wakiwemo wanazuoni wa Kiislamu, majaji, waandishi wa habari, na mawakili wanaoonekana kuwa wapinzani wa utawala huo wa kiukoo wanaendelea kuzuiliwa katika mazingira magumu katika jela za Aal-Saud.

Tags