Mar 03, 2022 11:19 UTC
  • Sisitizo la serikali ya Taliban la kufuatiliwa mafaili ya viongozi wa zamani wa Afghanistan

Rais wa serikali ya mpito ya Afghanistan ametoa wito wa kufuatiliwa mafaili ya viongozi wa serikali ya zamani ya nchi hiyo.

Mullah Muhammad Hassan Akhund, Rais wa serikali ya mpito ya Afghanistan ametoa wito huo katika kikao cha Baraza la Mawaziri ambapo sanjari na kuashiria mafaili ya ufisadi wa fedha wa viongozi wa serikali ya zamani ya Afghanistan amesema kuwa, amempa jukumu Mwanasheria Mkuu kufuatilia mafaili hayo.

Muhammad Khalid Hanafi, Kaimu wa Wizara ya Kuamrisha Mema na Kukataza Mabaya wa serikali ya Taliban hivi karibuni aliwatuhumu viongozi wa serikali ya zamani ya nchi hiyo kwamba, wamehusika na ufisadi wa fedha na kusema kuwa, Hamid Karzai, Rais wa zamani wa Afghanistan, Abdullah Abdullah, Mkuu wa zamani wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan na Fazal Hadi Muslimyar, Spika wa zamani wa Baraza la Seneti la Afghanistan kuwa ndio mapapa na manyangumi wa ufisadi wa kiuchumi nchini Afghanistan.

Sisitizo la Rais wa serikali ya mpito ya Taliban juu ya kufuatiliwa mafaili ya ufisadi ya viongozi wa serikali ya zamani ya nchi hiyo linatolewa katika hali ambayo, mara tu baada ya kushika hatamu za uongozi tena nchini humo Agosti mwaka jana, kundi la Taliban lilitangaza msamaha kwa wote kwa wafanyakazi na viongozi wote wa serikali ya zamani ya nchi hiyo.

Hamid Karzai Rais wa zamani wa Afghanistan

 

Hata baada ya Taliban kutangaza msamaha kwa wote nchini Afghanistan kulikuweko na shaka baina ya wananchi na vyombo vya habari vya nchi hiyo kuhusiana na msamaha huo kujumuisha viongozi wa zamani wa nchi hiyo. Baadhi ya viongozi wa serikali ya Taliban walijitokeza na kutangaza bayana kwamba, agizo hilo la msamaha litajumisha maafisa na viongozi wote wa zamani wa Afghanistan.

Baada ya kupita miezi sita tangu wanamgambo wa Taliban walipotangaza msamaha kwa wote nchini Afghanistan, matamshi ya Rais wa serikali ya mpito ya Taliban ya ulazima wa kufuatiliwa mafaili ya kimahakama ya viongozi wa serikali ya zamani ya nchi hiyo imewafanya wananchi waamini kwamba, kundi hilo halijaheshimu ahadi na agizo lake hilo.

Hata hivyo kundi la baadhi ya viongozi wa zamani wa Afghanistan waliokimbilia nje baada ya Taliban kushika hatamu za uongozi, hawana shauku ya kurejea nyumbani kutokana na kutokuwa na imani na kutekelezwa kivitendo agizo la msamaha kwa wote.

Kama alivyotangaza, Kaimu wa Wizara ya Kuamrisha Mema na Kukataza Mabaya  ya Afghanistan ni kuwa, mafaili ya ufisadi wa kiuchumi ya baadhi ya viongozi wa serikali ya zamani akiwemo Hamid Karzai, Abdullah Abdullah na Fazal Hadi Muslimyar ambao wapo ndani ya nchi hiyo yataaanza kushughulikiwa, hatua ambayo bila shaka inakinzana wazi na tangazo la awali la wanamgambo wa Taliban la msamaha kwa wote hata wafanyakazi wa serikali na viongozi wa serikali iliyopita, tangazo ambalo lilitolewa mwanzoni tu baada ya wanamgambo hao kushika hatamu za uongozi wa nchi.

Wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa Taliban

 

Hata hivyo, ukiukakaji wa msamahah kwa wote umeshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni kama zinavyovichua baadhi ya duru za habari ambapo wanamgambo wa Taliban wamewachukulia hatua baadhi ya viongozi wa serikali ya zamani ya nchi hiyo, hatua ambazo zinaonyesha kuwa, agizo la msamaha kwa wote halina itibari yoyote katika serikali ya Taliban.

Qassim Mozaffari, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan anasema: Baada ya Mullah Haibatullah, kkiongozi wa Taliban kutoa amri ya msamaha kwa wote, wananchi wa Afghanistan walikuwa wakidhani kwamba, vikosi vya Taliban vitaheshimu na kufungamana na agizo la kiongozi wao; hata hivyo hatua ya askari hao ya kutotekeleza agizo la Haibatullah limevunjia heshima pia nafasi ya kiongozi wao.

Katika mazingira ambayo, mafaili ya ufisadi wa kiuchumi ya viongozi wa zamani waandamizii wa Afghanistan yanatarajiwa kushughulikiwa na mahakama, kumeibuka wasiwasi huu kwamba, maagizo na amri nyingine za Taliban nazo yamkini zikakumbwa na hatima kama ya agizo la msamaha kwa wote, jambo ambalo kama litatokea linaweza kuipa nguvu misimamo ya mataifa mbalimbali ya kutoutambua rasmi utawala wa Taliban nchini Afghanistan.

Tags