Apr 03, 2022 08:17 UTC
  • Onyo la HAMAS kwa Israel baada ya kuwaua shahidi Wapalestina 3 Jenin

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imelionya vikali jeshi katili la utawala haramu wa Israel kwa kuwaua shahidi vijana watatu wa Kipalestina katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani huko Jenin.

HAMAS ilitoa indhari hiyo jana Jumamosi katika taarifa na kueleza kuwa: Huku tukiwaomboleza wanajihadi wetu waliouawa kioga na Israel, tunasisitiza kuwa sera ya mauaji ya kigaidi ya Israel kamwe haiwezi kuupa usalama utawala huo, wala kuhalalisha ukaliaji wake wa mabavu wa ardhi za Wapalestina.

Taarifa ya harakati hiyo ya muqawama imebainisha kuwa, "Jinai za aina hiyo hazina matokeo mengine ghairi ya kuipa nguvu na kushajiisha azma ya watu wa Palestina ya kuihami ardhi yetu na maeneo matukufu."

Wakati huouo,  Nabil Abu Rudeinah, msemaji wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas ameyataja mauaji hayo ya Jenin kama tishio na ukiukaji wa kanuni na sheria za kimataifa.

Mashahidi wa Palestina waliouawa alfajiri ya kwanza ya Ramadhani huko Jenin

Wapalestina hao waliuawa shahidi alfajiri ya jana baada ya gari lililokuwa limewabeba kumiminiwa risasi na wanajeshi wa Israel, karibu na lango la kuingia mji wa Arraba, kusini magharibi mwa Jenin.

Makundi ya muqawama ya Palestina yanasisitiza kuwa, operesheni za hivi karibuni za wanajihadi wa Kipalestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ni jibu kwa jinai za utawala huo pandikizi na hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Tags