Apr 04, 2022 02:34 UTC
  • Taliban yapiga marufuku uzalishaji wa mihadarati nchini Afghanistan

Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imepasisha sheria ya kupiga marufuku kilimo cha mipopi na uzalishaji wa aina nyingine zote za dawa za kulevya.

Dikrii hiyo iliyopasishwa na kiongozi wa Imarati ya Kiislamu ya Taliban imeeleza kuwa, kilimo cha zao la mpopi, uzalishaji wa dawa za kulevya na utumiaji wake ni haramu na kinyume na sheria za dini ya Kiislamu.

Amri hiyo mpya ya serikali ya Taliban imesema yeyote atakayekiuka sheria hiyo nchini Afghanistan atachukuliwa hatua kali na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.

Kadhalika sheria hiyo mpya mbali na kuzipiga marufuku kampuni za kuzalisha dawa za kulevya nchini Afghanistan, lakini imeharamisha pia utumiaji, usafirishaji, ununuzi na uuzaji wa mihadarati ndani na nje nchi.

Askari wa US walivyokuwa wakilinda mashamba ya mihadarati Afghanistan kabla ya kutimuliwa

Mwishoni mwa mwaka jana, jarida la Bloomberg lilisema katika ripoti yake kuwa, uzalishaji wa dawa za kulevya umeendelea kuongezeka nchini Afghanistan, na hivi sasa asilimia 87 ya mihadarati inayotokana na mmea wa mpopi (opium)  duniani, inazalishwa nchini humo.

Uzalishaji wa mihadarati ulikuwa umeshamiri Afghanistan kwa kuwa madola vamizi ikiwemo Marekani ndiyo yaliyokuwa yanadhibiti kila kitu nchini humo kwa muda wa miaka 20.

Tags