Apr 07, 2022 13:43 UTC
  • Israel yashadidisha kamatakamata dhidi ya Wapalestina mwezi huu wa Ramadhani

Vikosi vya utawala haramu wa Israel vimewashambulia Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuwatia mbaroni 13 miongoni mwao.

Shirika la habari la Wafa la Palestina limeripoti hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, askari wa utawala wa Kizayuni walifanya operesheni hiyo ya kamatakamata usiku wa kuamkia katika mji wa Ramallah na miji inayopakana nao kama vile al-Bireh.

Habari zaidi zinasema kuwa, Wapalestina wengine wamekamatwa katika mji wa Nablus, baadhi katika kambi ya wakimbizi ya Jalazone kaskazini mwa Ramallah, na wengine katika kambi ya al-Am'ari, kusini mwa mji wa al-Bireh.

Inaarifiwa kuwa, wanajeshi makatili wa Israel walishambulia nyumba za Wapalestina hao waliokuwa na jamaa zao kabla ya kuwakamata kwa mabavu na idhilali.

Haya yanajiri siku chache baada ya Wapalestina wawili kuwaangamiza askari wawili wa utawala ghasibu wa Israel na kujeruhi wengine wanne, kabla ya wao kuuawa shahidi kaskazini mwa mji wa Hadera unaokaliwa kwa mabavu.

Kuongezeka misako ya usiku ya Israel katika ardhi za Palestina zilizoghusubiwa

Vikosi vya Israel vimekuwa vikizidisha  ghasia na hujuma dhidi ya Wapalestina wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Jumamosi iliyopita, polisi wa Israel waliwatia mbaroni Wapalestina wanne katika usiku uliojaa ghasia na mvutano katika mji mkongwe wa al-Quds.

 

Tags