Apr 10, 2022 11:08 UTC
  • Iraq: Kambi ya Marekani inayowahifadhi magaidi mashariki mwa Syria inapaswa kuvunjwa

Afisa wa ngazi ya juu wa usalama wa Iraq ametoa wito wa kuvunjwa kambi ya wakimbizi inayodhibitiwa na wanamgambo wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani karibu na mpaka wa Iraq nchini Syria, akisema kambi hiyo inayohifadhi maelfu ya magaidi wa Daesh ni tishio halisi kwa nchi yake.

Qasim al-Araji ameuambia mkutano wa kimataifa kuhusu kambi hiyo uliofanyika Baghdad kwamba: "Kuwepo kwa kambi ya al-Hawl Mashariki mwa Syria ni tishio halisi kwa sababu ya uwepo wa magaidi 12,000 ndani yake, na magaidi wa Daesh wanajaribi kupenya kwenye kambi hiyo."

Kambi hiyo iko katika viunga vya Kusini mwa mji wa al-Hawl katika mkoa wa al-Hasakah nchini Syria, ambapo vikosi vamizi vya Marekani na washirika wake wanaendeshea shughuli zao. 

Hiyo ndiyo kambi kubwa zaidi ya wakimbizi katika nchi ya Syria iliyokumbwa na vita, ikiwa na zaidi ya watu 60,000 kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Pia kuna ripoti zinazosema kuwa magaidi wa Daesh wanatumia kambi hiyo kwa madhumuni ya kusajili wapiganaji wapya.

Kwa sababu hiyo, afisa huyo wa ngazi ya juu wa Iraq ametoa wito kwa nchi za kigeni kuwarejesha makwao raia wao walioko kwenye kambi ya wakimbizi ya al-Hawl na kuhimiza kuvunjwa kwa kambi hiyo haraka iwezekanavyo.

"Magaidi wote katika kambi ya al-Hawl lazima wahamishwe na kupelekwa katika nchi zao kwa ajili ya kufunguliwa kesi", amesisitiza al-Araji.

Siku kadhaa zilizopita, al Araji alifanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Iraq, Matthew Tueller kuhusiana na kadhia hiyo.

Iraq ilitangaza ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh mnamo Desemba 2017 baada ya mapambano ya miaka mitatu ya kijeshi dhidi ya ugaidi, ambayo yalisaidiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags