Apr 12, 2022 07:48 UTC
  • Jihad Islami: Siku zilizobaki za Ramadhani ni uwanja wa vita vikali na wavamizi

Mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema kuwa, siku zilizosalia za mwezi mtukufu wa Ramadhani zitakuwa uwanja wa vita vikali na wavamizi wanaoikalia Quds kwa mabavu na kuongeza kuwa, ujinga wowote wa utawala ghasibu wa Israel utauangamiza utawala huo.

Tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha mashinikizo na jinai zake dhidi ya watu wa Palestina jambo ambalo limepelekea kuongezeka mapambano wa Wapalestina dhidi ya uvamizi na kuzidisha wimbi jipya la operesheni za kujitolea kufa shahidi.

Mohammad Shalh, mwanachama mwandamizi wa harakati ya Jihad ya Islami ya Palestina amesema: "Uwanja wa vita kati ya wananchi wa Palestina na utawala wa Kizayuni bado uko wazi, na mapigano yanaendelea katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hususan huko Jenin."

Shalh ameongeza kuwa Jenin ndio chimbuko la watu wakubwa, mapambano na vuguvugu la mapinduzi katika Ukingo wa Magharibi, na ndio maana wavamizi wanataka kulipiza kisasi kwa watu wa eneo hilo.

Wanamapambano wa Kipalestina

Mwanachama huyo wa ngazi ya juu wa harakati ya Jihad ya Islami amesema kwamba utawala unaoukalia kwa mabavu Quds tukufu unatumia njia maalumu kutokomeza kambi ya Jenin, lakini hiyo haina maana kwamba watu wa Jenin watainua mikono juu ya kujisalimisha.

Jumapili iliyopita wanajeshi wa Israel walishambulia miji na vijiji kadhaa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, vikiwemo Jenin, Nablus, Tulkarm na Jeriko na kuwafyatulia risasi raia wa maeneo hayo. Wapalestika watatu akiwemo Ghada Ibrahim Sabatin, 47, mama wa watoto sita, wameuwa shahidi katika mashambulizi hayo ya wanajeshi wa Israel yaliyopamba moto sambamba na kuanza mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Tags