Apr 17, 2022 07:53 UTC
  • Mkuu wa zamani wa ujasusi wa Israel: Bin Salman anaitazama Tel Aviv kama mshirika

Aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Jeshi la utawala haramu wa Israel amesema Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia anaitazama Tel Aviv kama mshirika wake wa karibu.

Jenerali Amos Yadlin alisema hayo katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya kanali ya 12 ya televisheni ya Kizayuni, ambapo amesisitizia haja ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala huo pandikizi na utawala wa kiukoo wa Aal-Saud.

Amedai kuwa, kuanzishwa uhusiano huo kutaimarisha ushawishi na nafasi ya Israel katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi), na pia kuilazimisha Marekani iwe na misimamo mikali dhidi ya Iran hususan dhidi ya miradi ya nyuklia ya Tehran. 

Februari mwaka huu pia, kanali ya 12 ya televisheni ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel imetangaza kuwa, Bin Salman anafuatilia suala la kuunganisha Uyahudi katika utamaduni wa asili wa nchi yake na anataka Saudia na Israel ziwe na uhusiano wa kawaida na wa wazi.

Kanali hiyo ya televisheni mbali na kupongeza siasa za mrithi huyo kijana wa kiti cha ufalme wa Saudia ambaye kimsingi kwa sasa ndiye mtawala wa Saudia imesisitiza kuwa, Bin Salman anafanya juhudi za kubadilisha kikamilifu utambulisho wa Saudi Arabia.

Sehemu nyingine ya ripoti ya televisheni hiyo ya Israel ilieleza kwamba, Muhammad bin Salman anakusudia kuitenganisha Saudia na sheria za Kiislamu.

Tags