Apr 17, 2022 08:17 UTC
  • Wamorocco, Wabahrain, Waturuki waandamana kuitetea Aqsa, Syria, Kuwait zatoa kauli

Wananchi wa Morocco wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Rabat kutangaza uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina, sanjari na kulaani kitendo cha utawala haramu wa Israel cha kuuvamia na kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa.

Wananchi wa Morocco walikusanyika mbele ya Bunge la nchi hiyo katika maandamano hayo ya jana Jumamosi, huku wakipiga nara za kuulani jinai hizo mpya za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.

Waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kuonyesha mshikamano wao kwa wananchi madhulumu wa Palestina, na kulaani kitendo cha kishenzi cha Wazayuni cha kuvunjia heshima Masjidul Aqsa ulioko katika mji mtukufu wa Quds, katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco imetoa taarifa ya kukosoa hatua ya askari wa utawala haramu wa Israel ya kuwashambulia Wapalestina ndani ya Msikiti wa al-Aqsa mjini Quds (Jerusalem) ambapo zaidi ya waumini 220 walijeruhiwa, mbali na wengine 400 kutiwa mbaroni.

Huku hayo yakiarifiwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imelaani pia uvamizi huo wa Msikiti Mtukufu wa Aqsa juzi Ijumaa na kusisitiza kuwa, ina wasiwasi mkubwa kutokana na matukio hayo hasasi yanayoshuhudiwa huko Palestina.

Waturuki katika maandamano ya kuitetea Quds

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, mashambulio hayo ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina ndani ya Msikiti wa Aqsa, tena katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ni uchokozi wa wazi unaoweza kufanya hali mambo katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu kuwa mbaya zaidi.

Kadhalika wananchi Waislamu na wapenda haki katika nchi za Bahrain, Uturuki na Iraq wamemiminika mabarabarani katika maandamano ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matukufu. 

Aidha Spika wa Bunge la Kuwait, Marzouq Al-Ghanim ameitaka jamii ya kimataifa isimame na kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina katika juhudi zao za ukombozi.

Tags