Apr 21, 2022 02:49 UTC
  • Mufti wa Oman awakosoa viongozi wa Kiarabu wanaofuturu na Wazayuni huku al Aqsa ikitiwa najisi

Mufti Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmed bin Hamad al-Khalili, amepongeza misimamo ya kishujaa ya wanamapambano wanaoendelea kukabiliana na uvamizi wa mara kwa mara wa Israel katika Msikiti wa Al-Aqsa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Sheikh Ahmed Al-Khalili amesema katika ujumbe uliowekwa kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Kama tunavyofurahishwa na kustaajabia msimamo wa kishujaa uliochukuliwa na wanamapambano huko Quds tukufu kwa ajili ya kuulinda msikiti huo usitiwe najisi na utawala wa Kizayuni, vilevile tunanyenyekea na kumuomba Mwenyezi Mungu awape nusra mashujaa hawa, na awatia nguvu kwa Malaika Wake."

Mufti wa Oman amekosoa usaliti wa Umma wa Kiislamu, hususan Waarabu, na kutowasaidia ndugu zao huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na amewakemea ya baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu kwa kukubali kudhalilishwa na kujidunisha na kukimbilia kuketi kwenye meza ya futari ya Wazayuni! "Lini Umma huu utapona maradhi haya?, amehoji Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed bin Hamad Al-Khalili.

Askari wa Israel wavamia Msikiti wa al Aqsa

Siku chache zilizopita Rais wa utawala haramu wa Israel, Isaac Herzog, aliwaalika nyumbani kwake kwenye meza ya futari mabalozi wa nchi za kigeni, wakiwemo mabalozi wa Misri, Jordan, Bahrain, Imarati na Morocco .

Tangu mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani Wapalestina wasiopungua karibu 20 wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala ghasibu wa Israel. 

Tags