Apr 25, 2022 10:42 UTC
  • Mrengo wa Sadr waandaa muswada wa kupiga marufuku uhusiano na Israel

Mrengo wa Sadr unaoongozwa na mwanachuoni mashuhuri wa Kishia nchini Iraq, Muqtada al-Sadr umeandaa muswada wa sheria inayoharamisha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Sadr amebainisha kuwa: Harakati ya Sadr na waitifaki wake karibuni watatangaza muswada wa kufanya kuwa jinai uanzishwaji wa uhusiano wa kawaida na kuwa na muamala wowote na utawala wa Kizayuni.

Kiongozi huyo mashuhuri wa Waislamu wa madhehebu ya Shia amesema maandalizi yakishakamilika, muswada huo utapelekwa Bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura.

Muqtada al-Sadr ameeleza bayana kuwa, "Suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, na ndoto za utawala huo haramu kutaka kulitawala taifa letu pendwa la Iraq, ni moja ya sababu kuu za Harakati ya Sadr kujitosa kwenye mchakato wa uchaguzi."

Sayyid Muqtada al-Sadr

Itakumbukwa kuwa, muungano wa Sadr ulishinda zaidi ya viti 70 katika uchaguzi wa Bunge la Iraq uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana 2021. 

Kiongozi huyo mashuhuri wa Kishia nchini Iraq huko nyuma pia alilaani mkutano uliofanyika Septemba mwaka jana katika eneo la Kurdistan la Iraq kwa lengo la kushinikiza kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel na akasisitiza kuwa, "Erbil inapaswa kuharamisha mikusanyiko ya aina hiyo ya Wazayuni magaidi."

 

Tags