May 04, 2022 02:36 UTC
  • Ujumbe wa Idi wa makundi ya muqawama: Mapambano dhidi ya mabeberu yataendelea

Brigedi za Hizbullah nchini Iraq zimesema kuwa, zitaendeleza muqawama na kushikamana vilivyo na Uislamu hadi pale ubeberu wa madola ya Magharibi utakapoangamizwa katika nchi za Waislamu.

Kwa mujibu wa al Ittijah, brigedi za Hizbullah za nchini Iraq zilisema hayo jana Jumanne katika ujumbe wao wa Idul Fitr na mbali na kutoa mkono wa baraka za Idi kwa wananchi wa Iraq na wanajihadi mashujaa zimesema kuwa, hamu yake kubwa ni kuuona umma wa Kiislamu unaishi kwenye usalama na amani, utulivu na ustawi katika nyanja na nyuga zote.

Kwenye ujumbe wao huo wa Idi, brigedi hizo zimetilia mkazo kuendelea kushikamana na muqawama na mafundisho ya Uislamu na kusisitizia vipaumbele vyake vikuu hasa vya kupambana na nembo za dhulma, kuwasaidia na kuwaunga mkono wanyonge na wanaudhulumiwa na kulinda haki zao.

Sheikh Nabil Qawuq

 

Kwa upande wake, Sheikh Nabil Qawuq, mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, bendera ya muqawama itaendelea kupepea licha ya kuweko njama nyingi za kila upande za kujaribu kuishusha chini.

Amesema, Hizbullah ya Lebanon itaendelea kutekeleza jukumu lake la kidini, kibinadamu na kitaifa la kulinda ardhi yote ya Lebanon na usalama wa wananchi wa nchi hiyo kama ambavyo pia itaendelea kujiimarisha kijeshi ili kuondoa kabisa uwezekano wa adui kulivamia na kulishambulia taifa la Lebanon.

Aidha amesema, njama zote za Marekani na vibaraka wake za kujaribu kusambaratisha muqawama wa wananchi wa Lebanon zimefeli huku wananchi wa nchi hiyo wakizidi kushikamana na muqawama na Hizbullah siku baada ya siku.

Tags