May 04, 2022 11:52 UTC
  • HAMAS: Operesheni ya Ari'el ni kuwazindua Wazayuni wasivuke mstari mwekundu

Kiongozi mmoja wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Msikiti wa al Aqsa ni mstari mwekundu kwa Wapalestina na kwamba Wazayuni hawapaswi kuuvuuka.

Televisheni ya al Manar imemnukuu Jasir al Barghouthi, mmoja wa viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS akisema hayo na kuongeza kuwa, Brigedi za Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la harakati hilo ndilo lililofanya operesheni ya Ari'el ili kuwazindua Wazayuni kuwa Msikiti wa al Aqsa ni mstari mwekundu kwa kila Mpalestina na kwamba walowezi wa Kizayuni popote walipo hawatokuwa salama maadamu utawala wa Kizayuni unaendelea kuvuka mistari hiyo myekundu.

Ikumbukwe kuwa, Ijumaa usiku, kulitokea mapigano ya silaha karibu na kitongoji cha walowezi wa Kizayuni cha Ari'el huko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Operesheni hiyo ilifanywa na Wapalestina wawili. Askari mmoja Mzayuni ameangamizwa kwenye operesheni hiyo.

Brigedi za Izzuddin Qassam, Tawi la Kijeshi la HAMAS

 

Kiongozi huyo wa HAMAS pia amesema, harakati hiyo imejiweka tayari muda wote kulinda malengo matukufu ya taifa la Palestina kikiwemo Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa. Amesema, jambo lolote linalohusiana na masuala ya usalama wa Wapalestina na matukufu yao, harakati ya HAMAS haiwezi kulifumbia macho hata kwa sekunde moja.

Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS pia limesema kuwa, operesheni hiyo ya Ari'el dhidi ya walowezi wa Kizayuni, haitokuwa ya mwisho.

Tags