May 10, 2022 02:28 UTC
  • Usitishaji vita; igizo la usanii inaofanya Saudia Yemen kwa kuutumia vibaya Umoja wa Mataifa

Awamu ya kwanza ya ubadilishanaji mateka kati ya Yemen na Saudi Arabia imefanyika katika hali ambayo Riyadh ingali inazuia kufunguliwa tena Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a.

Hans Grundberg, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen alitangaza usitishaji vita wa muda wa miezi miwili katika vita vya Yemen, ambao ulianza kutekelezwa tarehe Pili ya mwezi uliopita wa Aprili. Siku 36 zimepita tangu usitishaji huo wa mapigano ulipoanza kutekelezwa. Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Grundberg, pande mbili hasimu zilikubaliana kuhusu kuingia meli za fueli katika bandari ya Al-Hudaydah magharibi ya Yemen, kubadilishana mateka wa vita pamoja na kufanyika safari za ndege za kibiashara za kuingia na kutoka uwanja wa ndege wa Sana'a kuelekea viwanja maalumu vya ndege katika eneo.

Hans Grundberg

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen, lengo la usitishaji vita lilikuwa ni kutoa fursa kwa wananchi wa Yemen ya kupumua kutokana na machafuko na mateso wanayopata; na muhimu zaidi ya hilo, kuleta matumaini ya kuhitimishwa vita nchini humo.

 Zikiwa zimeshapita siku 36, moja ya vipengee vya makubaliano ya usitishaji vita, yaani ubadilishanaji wa mateka kilitekelezwa siku ya Ijumaa iliyopita ya tarehe 6 Mei. Pamoja na hayo, nukta moja ya msingi iliyopo ni kwamba, baada ya kufanyika zoezi hilo imebainika kuwa Saudia iliwapa mateso makali mateka wa kivita wa Yemen. Ali Ad-Daylami, kaimu waziri wa haki za binadamu wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen alitangaza siku ya Jumamosi kuwa, maafisa wa nchi hiyo wana wasiwasi juu ya hali za mateka na kwamba taarifa walizonazo zinaonyesha kuwa, mateka wa nchi hiyo wameteswa.

Suala jengine ni kwamba wakati muhula wa miezi miwili ya usitishaji vita unakaribia kwisha, vipengee viwili muhimu, yaani kufunguliwa tena uwanja wa ndege wa Sana'a na kuingia meli za fueli katika bandari ya Al-Hudaydah bado havijatekelezwa ipasavyo. 

Bandari ya Al-Hudaydah

Saudi Arabia, ambayo ilitoa ahadi mara kadhaa ya kuruhusu kufuguliwa tena uwanja wa ndege wa Sana'a, zikiwa zimeshapita siku 36, bado haijatekeleza ahadi hiyo. Siku chache nyuma, Muhammad Abdusalam, msemaji wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen, alitoa taarifa maalumu kwa mnasaba wa kumalizika mwezi mmoja wa kutekelezwa usitishaji mapigano na akabainisha kuwa, mwezi mmoja wa usitishaji vita kwa sababu za kibinadamu nchini Yemen umepita, lakini ndege hazijaruhusiwa kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Sana'a.

Wakati huohuo, kipengee cha kuruhusu meli za mafuta kuingia bandari ya Al-Hudaydah nacho pia hakijatekelezwa kikamilifu; na upande wa Saudia ungali unazuia meli hizo kuingia nchini Yemen. Kuhusiana na suala hilo shirika la mafuta la Yemen lilitangaza siku ya Jumamosi kuwa, muungano vamizi wa Saudia uliizuia meli moja iliyobeba dizeli na kuipeleka kwa nguvu eneo la al Hajz katika pwani ya Jizan. Shirika hilo limesisitiza kuwa, muungano wa kijeshi wa Saudia umechukua hatua hiyo ilhali meli hiyo ilikuwa imefanyiwa upekuzi na kupewa kibali pia na Umoja wa Mataifa cha kuingia nchini Yemen.

Meli za fueli zinazuiliwa kuingia Al-Hudaydah katika hali ambayo, kwa mujibu wa msemaji wa shirika la mafuta la Yemen Essam al-Mutawakkil sekta muhimu na za utoaji huduma za nchi hiyo zinahitaji mno na kwa haraka nishati ya fueli. Si hayo tu, kuzuiliwa ndege kuruka katika uwanja wa ndege wa Sana'a kumeplekea hali mbaya ya kibinadamu iendelee kushuhudiwa nchini Yemen.

Duru za Yemen zimetangaza kuwa, katika kipindi cha mwezi mmoja tu wa kwanza wa usitishaji vita wa miezi miwili uliotangazwa na Umoja wa Mataifa, kuendelea kwa mzingiro na kufungwa uwanja wa ndege wa Sana'a na muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia, kumesababisha vifo vya wagonjwa 12 waliokuwa wakihitaji kupelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Kwa kuzingatia yote hayo, maafisa wa Yemen wanaitakidi kuwa, usitishaji vita wa miezi miwili, ni usanii na maonyesho tu yanayofanywa na Saudi Arabia kwa msaada wa Umoja wa Mataifa. Ali Ad-Daylami, kaimu waziri wa haki za binadamu wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen amesema kuhusiana na suala hilo kwamba, muungano wa Saudia unautumia Umoja wa Mataifa kwa manufaa yake. Ali al-Qahum, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen naye pia amesema, tokea awali, muungano wa Saudia haukuheshimu makubaliano ya usitishaji vita, kwa sababu usitishaji vita huo uliwekwa kwa msingi wa kuitilia maanani hali ya kibinadamu na suala la mateka, lakini muungano vamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia unafanya kila mbinu kukwamisha na kufelisha juhudi zote zinazofanywa ili kudumisha usitishaji vita huo.../

Tags