May 10, 2022 04:13 UTC
  • Barhum Salih asisitiza udharura wa kukabiliana na ugaidi na vitisho vya usalama

Rais wa Iraq amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo ambapo amemueleza kuhusu hatua za karibuni za kupambana na masalia ya kundi la kigaidi la Daesh .

Mabaki ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh waliyodhoofishwa yangali yanatekeleza hujuma za kigaidi katika baadhi ya maeneo ya Iraq licha ya kusambaratishwa kundi hilo mwezi Novemba mwaka 2017. 

Katika mazungumzo hayo na Inad Juma Waziri wa Ulinzi wa Iraq, Rais Barhum Salih amesisitiza juu ya udharura wa kuwa macho, kuwa makini na kutotoa mwanya kwa magaidi kufanya njama na kutishia amani na usalama wa watu wa Iraq. 

Rais wa Iraq amepongeza pia jitihada za karibuni za vikosi vya usalama vya nchi hiyo katika kusambaratisha mabaki ya magaidi na kuwatia nguvuni baadhi yao waliotambuliwa. Amesema kuna haja ya kuendeleza mashinikizo dhidi ya magaidi na wakati huo huo kutoa msaada wa pande zote kwa vikosi vya usalama ili viweze kutekeleza ipasavyo majukumu yao katika uwanja huo. 

Naye Waziri wa Ulinzi wa Iraq Inad Juma amemueleza Rais Barhum Salih kuhusu operesheni mbalimbali za kijeshi zilizoendeshwa katika medani tofauti katika vita dhidi ya masalia ya magaidi wa Daesh ambao wanafanya kila wanaloweza kuvuruga amani na utulivu katika miji na mikoa mbalimbali ya Iraq. 

Magaidi wa Daesh (ISIS)

 

Tags