May 11, 2022 10:42 UTC
  • Ukosoaji wa Sayyid Nasrullah kwa wanaoziandama silaha za muqawama badala ya matatizo ya uchumi, katika kampeni za uchaguzi wa Lebanon

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah, amesema kuhusu matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na vituo kadhaa vya utafiti kwamba dukuduku la akthari ya watu wa Lebanon si silaha za Muqawama bali ni hali zao za maisha.

Uchaguzi wa Bunge la Lebanon utafanyika nchi nzima tarehe 15 ya mwezi huu wa Mei. Uchaguzi huo kwa Walebanon walioko nje ya nchi ulifanyika hapo kabla kwa muda wa siku mbili. Katika siku za karibuni, kampeni za uchaguzi huo zimepamba moto zaidi. Wakati ripoti ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa Lebanon inakabiliwa na mgogoro na hali mbaya zaidi ya kiuchumi kuwahi kushuhudiwa katika muda wa karne moja sasa, katika kampeni zao, baadhi ya makundi na mirengo ya nchi hiyo imeacha kuipa umuhimu hali mbaya ya uchumi wa nchi, na badala yake kuziandama silaha za Muqawama kwa kutaka harakati ya Hizbullah ipokonywe silaha.

Mgogoro wa uchumi wa Lebanon umekuwa mkubwa kiasi ambacho, raia wa baadhi ya maeneo hasa Tripoli wanayatoroka makazi yao. Raia wengi wa Lebanon wamepoteza maisha wakati wakisafiri kwa kutumia boti kulihama eneo la Tripoli. Hali mbaya ya kiuchumi na hata kushindwa baadhi ya watu kujidhaminia mahitaji yao ya msingi ya maisha hasa chakula, ndio sababu ya raia hao kuyahama makazi yao.

Gazeti la Washington Post limeeleza katika ripoti kama ifuatavyo: "Viongozi wa Lebanon hawajashughulikia kile ambacho Benki ya Dunia imekielezea kama moja ya hali mbaya zaidi ya kiuchumi duniani; na Walebanon wamepoteza matumaini ya kupatiwa huduma kwa kuitegemea serikali. Tripoli, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa na umasikini nchini Lebanon, licha ya kuwa na eneo kubwa, na kuzingatia ukweli kwamba ndiko ziliko nyumba za baadhi ya matajiri wakubwa na shakhsia mashuhuri wa kisiasa wa nchi hiyo, akiwemo waziri mkuu wa sasa, haipewi msaada wala msukumo wowote."

Hali ya umasikini ya mji wa Tripoli

Hali hiyo inashuhudiwa pia katika baadhi ya maeneo mengine ya Lebanon. Lakini pamoja na hayo, baadhi ya makundi ya kisiasa na wagombea katika uchaguzi wa bunge wamejikita katika kupiga upatu dhidi ya silaha za Hizbullah, suala ambalo limekosolewa na Katibu Mkuu wa harakati hiyo Sayyid Hassan Nasrullah. Kiongozi huyo wa Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon amesema: "katika moja ya chunguzi za maoni zilizofanywa imebanika kuwa, lililo muhimu zaidi kwa wananchi ni suala la uchumi, maisha na ufisadi; na ni watu wachache ambao wamezungumzia silaha za muqawama; lakini kwa masikitiko, baadhi ya makundi ya kisiasa yamelishikilia suala hili ambalo ni la kipaumbele cha chini  kabisa." 

Nukta nyingine ni kwamba, baadhi ya makundi yanazisakama silaha za muqawama, wakati matukio ya ndani ya Lebanon yanaonyesha kuwa, silaha za muqawama zimetumika kikamilifu kulinda usalama wa nchi hiyo na pia dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Eneo la kusini mwa Lebanon ni mfano mmojawapo wa namna silaha za muqawama zilivyotumika kwa ajili ya kudhamini amani na usalama wa nchi hiyo. Kabla muqawama kuanzishwa kusini mwa Lebanon, eneo hilo lilikuwa likikaliwa kwa mabavu na jeshi la utawala ghasibu wa Israel na kutawaliwa na machafuko. Lakini kuanzia mwaka 2000 na kuendelea, eneo la kusini mwa Lebanon lilianza kushuhudia amani, heshima na usalama. Utawala wa Kizayuni uliyavamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya ardhi ya Lebanon kwa madhumuni ya kufanikisha mpango wake wa Israel Kubwa, lakini ulishindwa vibaya na Hizbullah na mpango wake huo ukagonga mwamba. 

Walebanon wa kusini wakisherehekea kutimuliwa kwa Israel na Muqawama wa Hizbullah katika ardhi zao

Kuhusiana na suala hili pia Sayyid Hassan Nasrullah amesema, baadhi ya watu wanataka muqawama upokonywe silaha, huku wakifumbia macho matunda na mafanikio yote ya kitaifa yaliyopatikana, ikiwemo kukombolewa maeneo yote ya Lebanon yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu; na akalifafanua hilo kwa kusema: "Wakati ule, adui Israel alikuwa ameikalia kusini yote kwa mabavu. Muqawama na makundi yake yote uliweza kuzikomboa ardhi za Lebanon zilizokuwa zimevamiwa; na kwa izza na heshima kamili, ukawakomboa pia mateka wote. Bila shaka wako baadhi ambao bado hawajulikani waliko; lakini Muqawama ulipigilia msumari jeneza la mpango wa Israel Kubwa."

Inavyoonekana, sababu kuu ya kupingwa silaha za muqawama na kuendeshwa kampeni kali dhidi yake inatokana na mambo mawili. La kwanza ni kuwa, silaha za muqawama zimeipatia Hizbullah itibari kitaifa na kupandisha hadhi na nafasi yake mbele ya wananchi wa Lebanon. Ushahidi wa hilo ni ushindi mkubwa uliopata muungano wa muqawama katika uchaguzi wa bunge wa mwaka 2018. Na jambo la pili ni kwamba, rai ya kutaka muqawama upokonywe silaha inatolewa na watu wanaoungwa mkono na wanaofuata muelekeo wa baadhi ya nchi za eneo za kambi ya wafanya mapatano na utawala wa Kizayuni, watu ambao ndani ya Lebanon pia wanataka uanzishwe uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu na ghasibu.../

Tags