May 14, 2022 02:12 UTC
  • Rasimu ya kupiga marufuku uhusiano wa kawaida na Israeli yapitishwa katika bunge la Iraq

Bunge la Iraq limeidhinisha rasimu ya sheria inayopiga marufuku kuanzisha au kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Rasimu hiyo inatoa adhabu ya kifo kwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuhusika na uhalifu huo.

Nchi za Kiarabu zilianza kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa kibaguzi wa Israel tangu Septemba 2020 kwa upatanishi au hata kwa kulazimishwa na utawala wa Doland Trump, rais wa zamani wa Marekani. Nchi nne za Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan zilianzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu unaoendelea kuikaliwa kwa mabavu Quds Tukufu mwaka 2020.

Karibu miaka miwili iliyopita, kumekuwepo na matukio mawili muhimu katika uhusiano wa nchi za Kiarabu na utawala huo wa Kizayuni.

Tukio la kwanza ni kuimarishwa uhusiano wa Imarati na Bahrain na utawala wa kibaguzi wa Israel ambapo nchi mbili hizo zimefungua balozi zao huko Tel Aviv nao utawala huo pia kufungua ubalozi wake katika miji mikuu ya nchi hizo, yaani Manama na Abu Dhabi. Katika kipindi hiki pia viongozi wa kisiasa wa pande tatu hizo wamekuwa wakitembeleana katika miji mikuu yao. Kwa msingi huo uhusiano wa Imarati na Bahrain na utawala ghasibu wa Israel si tu kuwa umebakia katika ngazi ya kufunguliwa balozi katika miji mikuu ya pande hizo bali watawala wa nchi hizo wamefanya kila wanaloweza kuimarisha uhusiano wao katika nyanja tofauti. Uhusiano wa Morocco na utawala huo haramu pia unaendelea kuimarika lakini uhusiano wa Sudan na utawala huo wa kibaguzi haujaimarika sana katika miaka miwili iliyopita.

Bunge la Iraq

Hatua ya pili ni kuvunjwa na kuvukwa mistari myekundu iliyokuwepo ya kuchukizwa nchi za Kiarabu kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo haramu. Saudi Arabia ni moja ya nchi za Kiarabu ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kukiuka jambo hilo. Kuhusu hilo, nchi hiyo imezipa ndege za utawala haramu kibali cha kupitia katika anga yake bila tatizo lolote. Hata kama nchi hiyo ya kifalme haijachukua hatua kama ile iliyochukuliwa na nchi kama Imarati au Bahrain katika kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel, lakini bila shaka uhusiano wa Riyadh na Tel Aviv umeimarika zaidi kuliko nchi nyingine yoyote ya Kiarabu.

Nukta nyingine ni kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita utawala haramu wa Israel umefanya juhudi kubwa za kuzishawishi nchi za Kiarabu zilizokuwa na nafasi muhimu katika kuunga mkono mrengo wa mapambano ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni, kurejea nyuma na kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo. Iraq na Lebanon ni nchi mbili za eneo ambazo utawala huo umezizingatia sana katika uwanja huo. Erbil, mji mkuu wa eneo lenye utawala wa ndani la Kurdistan nchini Iraq Oktoba mwaka uliopita, ilikuwa mwenyeji wa kikao cha kuunga mkono juhudi za kuimarisha uhusiano wa nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel. Pia juhudi zimefanyika kwa ajili ya kuleta mgawanyiko kati ya viongozi wa Iraq wanaopinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv ili kupata uungaji mkono wa baadhi ya viongozi hao katika uwanja huo.

Pamoja na juhudi hizo zote lakini nchi mbili hizo za Kiarabu zimekataa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu. Uwepo mkubwa na madhubuti wa makundi ya mapambano pamoja na jumuiya huru za kiraia katika nchi mbili hizo umezuia kabisa kufanikiwa juhudi za kuimarisha uhusiano na utawala wa Kizayuni katika ardhi za nchi hizo. Wakati huo huo Bunge la Iraq limepitisha rasimu ya kupiga marufuku juhudi zozote za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv na kutoa adhabu kali ya kifo kwa mtu yoyote atakayepatikana na kosa la kuunga mkono jambo hilo. Kwa mujibu wa rasimu hiyo uungaji mkono au ushirikiano wa aina yoyote na mashirika ya Kizayuni pia umepigwa marufuku.

Kwa hakika Bunge ka Iraq limepitisha rasimu hiyo kwa kuelewa vyema kwamba kuna baadhi ya watu katika nchi hiyo wanaofanya juhudi za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel kwa madhara ya watu wa Iraq na nchi nyingine za eneo.

Shireen Abu Akleh, mwandishi wa al-Jazeera aliyeuawa kikatili karibuni na utawala wa Israel

Mbali na Bunge, Wizara ya Utamaduni, Utalii na Turathi za Kale ya Iraq pia imetoa taarifa ikitangaza kuwa itaandaa Wiki ya Utamaduni kwa ajili ya kuwaunga mkono watu wa Palestina na vilevile kuandaa vikao kwa ajili ya kuunga mkono sheria ya kupiga marufuku juhudi za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kibaguzi wa Israel.

Hatua hiyo ya bunge la Iraq inaweza kuwa hatua muhimu katika kuzishawishi nchi nyingine za Kiarabu kuchukua hatua kama hiyo katika kuunga mkono taifa la Palestina. Harakati ya Jihad al-Islami ya Palestina imetoa taarifa ikisisitiza kwamba: "Hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na Bunge la Iraq katika kupiga marufuku juhudi za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni muhimu katika njia ya kukabiliana na jitihada za utawala huo ghasibu za kuwa na ushiwishi katika nchi za Kiarabu."

Jambo linaloongeza thamani na umuhimu wa hatua hiyo ni kuwa imechukuliwa katika hali ambayo utawala katili wa Israel umeongeza jinai zake dhidi ya watu wa Palestina ambapo hilo linaweza kuwa ni jibu muwafaka la kukabiliana na jinai iliyotekelezwa karibuni na utawala huo ya kumuua kinyama Shahidi Shireen Abu Akleh, mwandishi wa Kipalestina wa televisheni ya al-Jazeera ya nchini Qatar.

Tags